Gavana Tutuba:Tunafuatilia kwa karibu na tuna akiba ya kutosha fedha za kigeni

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema, benki hiyo imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa dola na sarafu nyingine za kigeni, na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu hauathiriwi sana na changamoto ambazo zinatokana na mambo mbalimbali duniani.
Ameyasema hayo leo Julai 17, 2023 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam katika mkutano na wafanyabiashara wa maduka ya ubadilishaji fedha za kigeni nchini.

"Natumia fursa hii kuwapongeza kwa mchango wenu katika kutoa huduma za kubadilisha fedha za kigeni kwa wananchi na kusaidia ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla. 

"Napenda kuwajulisha kuwa mjadala wa leo ni muhimu kwa maslahi ya biashara zenu, sekta ya fedha na kwa uchumi wa nchi yetu kwa ujumla,"amefafanua Gavana Tutuba.

Katika mkutano huo, wadau hao wamepata fursa ya kujadiliana juu ya namna bora zaidi ya kusimamia na kuendesha biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Benki Kuu. 

Gavana Tutuba amesema, lengo la kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi katika biashara na upatikanaji wa huduma hiyo muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho nchi nyingi duniani zimekumbwa na uhaba wa dola ya Marekani.

"Kama mnavyofahamu, uhaba wa dola ya Marekani umesababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mahitaji ya dola kutokana na uchumi kufunguka baada ya janga la UVIKO-19, vita kati ya Urusi na Ukraine iliyosababisha kupanda kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali ikiwemo usafirishaji, na hivyo kuongeza mahitaji ya dola."

Pia,Gavana Tutuba amesema, mambo mengine yaliyosababisha uhaba wa dola ni mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyosababisha mahitaji makubwa zaidi ya dola.

Sambamba na sera ya fedha ya Marekani (kupandisha riba) iliyovutia wawekezaji wengi kuwekeza dola zao Marekani na kusababisha uhaba katika mataifa mbalimbali duniani.

"Napenda kuwajulisha kuwa, licha ya changamoto hii ya kidunia, nchi yetu imeendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi isiyopungua minne. 

"Mathalani, tarehe 14 Julai 2023, nchi yetu ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni kiasi cha dola za Marekani bilioni 5.55, ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kwa takribani miezi mitano,"amefafanua Gavana Tutuba.

Mbali na hayo, Gavana Tutuba amesema,mafanikio hayo hayawafanyi wabweteke ndiyo maana wameitisha mkutano huu leo ili wajadiliane namna bora zaidi ya kuwafikishia wananchi huduma ya kubadilisha fedha za kigeni.

"Kama mnavyofahamu mnamo mwaka 2018/2019, Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya operesheni maalum nchini kwenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni. 

"Operesheni hizi zilifuatiwa na uchunguzi uliokuwa na lengo la kubaini maduka ambayo yalikuwa yanaendesha
biashara kinyume na kanuni na sheria za nchi. 

"Uchunguzi huu ulipelekea baadhi ya maduka kufutiwa leseni kutokana na kubainika kutozingatia matakwa ya sheria
na kanuni,"amesema Gavana Tutuba.

Aidha,amesema baada ya operesheni hizo, Benki Kuu ilichukua hatua kadhaa ikiwemo kufanya mapitio ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni kwa lengo la kurekebisha mapungufu yaliyogundulika. 

Katika kanuni mpya za mwaka 2019, amesema mtaji wa leseni ya daraja A uliokuwa shilingi milioni 300 ulifutwa na hivyo kubakiza aina moja tu ya leseni ambayo mtaji wake ulikuwa shilingi bilioni moja, iliyokuwa inatumika kwa leseni za daraja B.

Amesema, katika kipindi cha matumizi ya Kanuni za Kubadilisha Fedha za Kigeni za mwaka 2019, Benki Kuu imebaini changamoto kadhaa ambazo zimeathiri utoaji wa huduma hiyo nchini. 

Miongoni wa changamoto amesema, ni wawekezaji wengi kushindwa kukidhi matakwa ya kanuni hususani mtaji wa shilingi bilioni moja, hivyo kusababisha kuwepo kwa watoa huduma wachache. 

"Hali hii imepelekea upatikanaji hafifu au kukosekana kwa huduma hii katika baadhi ya maeneo yenye uhitaji huo.
Katika kukabiliana na changamoto hii, Benki Kuu ilifanya mkutano na wadau wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini mwezi Januari na Aprili 2023 ili kupata maoni ya namna ya kuboresha mazingira ya biashara hii,"amesema Gavana Tutuba.

Vilevile, Gavana Tutuba amesema, Benki Kuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikutana na wadau wa sekta ya hoteli Zanzibar mnamo mwezi Januari 2023 na kujadili namna ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo ya hoteli za kitalii.

"Baada ya kupokea maoni ya wadau mbalimbali, Benki Kuu ilianzisha mchakato wa kupitia upya Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za 2019 kwa lengo la kurekebisha baadhi ya masharti ili wawekezaji wengi
zaidi waweze kuhamasika kuanzisha biashara hiyo na wale waliokuwepo waweze kurejea katika biashara hii. 
"Marekebisho haya yanajumuisha kupunguza kiwango cha mtaji ili kuwawezesha wawekezaji wengi wazawa kufungua maduka mapya ya kubadilisha fedha za kigeni. 

"Aidha, kanuni mpya zinalenga kuweka utaratibu utakaowezesha hoteli za kitalii nchini kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kwa wateja wao,"amesema Gavana Tutuba.

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amesema pamoja na marekebisho ya kanuni, Benki Kuu inaendelea kuhamasisha benki na taasisi za fedha kuboresha utoaji wa huduma ya kubadilisha
fedha za kigeni. 

Amesema, hadi mwezi Juni 2023 benki za bishara zipatazo 37 zenye mtandao wa matawi zaidi ya 900 yaliyosambaa nchi nzima zimeendelea kutoa huduma hizo.

Gavana Tutuba amesema,pia jumla ya maduka ya kubadilisha fedha yapatayo nane yalikuwa yamepewa leseni. Maduka hayo yana jumla ya matawi 36 nchini kote. 

Pamoja na hali hiyo, Gavana Tutuba anafafanua kuwa, bado ipo changamoto ya huduma za kubadilisha fedha za kigeni kutokupatikana katika muda ambao zinahitajika zaidi hususani kuanzia saa tisa alasiri, siku za mwisho wa juma (Jumamosi na Jumapili) na sikukuu. 

"Hivyo,Benki Kuu inapenda kutoa rai kwa wadau wote kulitazama hili ili kuweza kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha kote nchini,"amesisitiza.

Amesema, Benki Kuu itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu elimu ya fedha ikiwemo madhara yatokanayo na ubadilishaji fedha za kigeni kupitia watoa huduma wasio rasmi. 

Wakati huo huo, Gavana Tutuba amesema Benki Kuu itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola nchini katika kupambana na wale wote wanajihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni rasmi inayotolewa na Benki Kuu.

"Benki Kuu inatoa rai kwa wadau wa sekta hii kutoa ushirikiano ikiwemo kutoa taarifa pale wanapobaini uwepo wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni isiyo rasmi.

"Naomba nirudie kuwafahamisha kuwa Benki Kuu imekuwa ikipata taarifa za kuwepo upungufu wa fedha za kigeni katika soko letu. 

"Kama nilivyosema hapo awali, ni kweli kuwa kuna upungufu wa fedha za kigeni katika nchi nyingi duniani kutokana na sababu nilizoziainisha. 

"Hata hivyo,naomba niwatoe hofu Watanzania kuwa upungufu huo haujafikia kiwango cha kutia hofu kama inavyoelezwa na baadhi ya wadau. Aidha, Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali na itaendelea kuchukua hatua mahsusi zenye lengo la kuhakikisha kuwa upungufu huo wa fedha za kigeni, ambao upo Dunia nzima,hauathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wetu. 

"Naomba niwahakikishie kuwa tuko makini na kwa nguvu za Mwenyezi Mungu tutavuka. Napenda kutoa shukrani za dhati kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kukuza sekta ya fedha na uchumi ujumla. 

"Pia natoa shukrani kwa ushirikiano mzuri mnaotupatia katika kutekeleza majukumu yetu.Natoa rai kwamba muendelee kudumisha ushirikiano huo ili tuweze kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kwa manufaa yetu na taifa letu kwa ujumla. 

"Kwa kufanya hivi tutakuwa tunamuunga mkono Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu unakua kwa kasi na wananchi wetu walio wengi wananufaika na ukuaji huo wa uchumi,"amefafanua kwa kina Gavana Tutuba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news