Kamishna Jenerali wa DCEA abisha hodi JNIA

DAR ES SALAAM-Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo leo Julai 21, 2023 amefanya ziara ya kikazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na kufanya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya uwanja huo kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya DCEA na JNIA.
Katika kikao hicho wamejadili na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na kuazimia mambo kadhaa yatakayosaidia kudhibiti usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya nchini.

Ziara ya leo ni miongoni mwa mikakati ya mamlaka hiyo kuhakikisha inashirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kuhakikisha hakuna upenyo wowote wa kuingiza au kusafirisha dawa za kulevya nchini kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Mara kwa mara Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amekuwa akifafanua kuwa, Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinaeleza kwamba, ni kosa kusafirisha dawa za kulevya, na mtu yoyote akithibitika kutenda kosa hilo atawajibishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 30 au kifungo cha maisha gerezani.
Pia, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo ambaye amekuwa akiongoza operesheni mbalimbali za kutokomeza dawa za kulevya nchini ikiwemo vijijini pia amekuwa akipita katika mipaka mbalimbali ya nchi kuhakikisha mianya yote inayoweza kutumika kuingiza au kusafirisha dawa za kulevya inadhibitiwa kwani, Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha inamaliza tatizo la dawa za kulevya nchini.

Aidha, mara nyingi amekuwa akisema, kutokana na kuwepo madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya, ni vema wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwafichua wote wanaojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
"Ni ili kwa pamoja tuweze kulikomboa taifa kutoka katika janga hili.Aidha, katika kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya yanatokomea nchini. Mamlaka imejikita katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa jamii."

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. 

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Majukumu

Majukumu ya Mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya. Katika kutekeleza majukumu hayo Mamlaka inafanya kazi zifuatazo:

i.Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya.
ii.Kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya.

iii.Kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii;

iv.Kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya;

v.Kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti;

vi.Kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.

vii.Kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi;

viii.Kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

ix.Kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa;

x.Kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya;

xi.Kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya;
xii.Kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xiii.Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu.

xiv.Kufanya uchunguzi wa sayansi jinai.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news