Rais Dkt.Mwinyi asisitiza umuhimu wa tafiti

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amehimiza jamii kufanya utafiti kwenye nyanja mbalimbali ili kutanua wigo na kukuza elimu kupitia sekta za maendeleo.

Alhajj Dkt.Mwinyi ametoa rai hiyo leo Julai 21, 2023 kwenye Masjid Abuu Ubayda, Fuoni Meli Saba, Mkoa wa Mjini Magharibi, alikojumuika na waumini wa dini ya Kiislamu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.

Amesema, mataifa makubwa yaliyoendelea yamewekeza mtaji mkubwa kwenye elimu, ambao hutumia fedha nyingi kushajihisha elimu.

Alhajj Dkt.Mwinyi alieleza kadri ya mataifa hayo yanavyotumia fedha nyingi kwenye elimu, ndivyo wanavyopiga hatua zaidi za maendeleo.

“Ukisikia kuna nchi inafanya maendeleo makubwa basi ujue ndani yake watu wamejikita mno katika masuala mazima ya elimu, suala la utafiti maana elimu inaletwa na utafiti.”

Amesema, elimu ndio inayoleta mabadiliko makubwa kwenye jamii maendeleo yote yanatokana na elimu watu kujifunza elimu ya dini na dunia.

Kwa upande mwingine Alhajj Dkt. Mwinyi alieleza elimu ya dini huwapandisha daraja waumini wake kwa kuendelea kumcha Mwenyezi Mungu kikweli katika kutekeleza ibada ya haki kama inavyotakiwa.

Pia, Alhajj Dkt.Mwinyi amewasihi wazazi na walezi kuendelea kuwahimiza watoto wao kusoma elimu zote mbili ya dini na dunia, ili kukuza taifa lenye vijana wenye maadili na busara ya kukimbilia maendeleo kwa ajili ya familia zao na taifa kwa ujumla.

Alieleza, miongoni mwa sababu zinazochangia mmong’onyoko wa maadili kwenye jamii ni ukosefu wa elimu zote mbili, hivyo aliiasa jamii kuweka mkazo zaidi kwenye elimu na kulinda maadili ya uislamu.

Hata hivyo, Alhajj Dkt. Mwinyi aliitaka jamii kuendelea kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata mafundisho ya Mtume (SAW) kwa kufanya yaliyo mema na kuacha mabaya yanayomchukiza Allah (S.W).

Naye Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, ameisisitiza jamii ya waislam kuendelea kukithirisha ibada hasa kwenye mwezi mtukufu wa Muharram.

Amesema, Mwezi wa Mfunguo nne (Muharami) ni miongoni mwa miezi mitukufu ya Mwenyezi Mungu baada ya Ramadhan. Pia alisisitiza mwezi 10 Muharam ni Sunna kufunga kwa waumini wa dini ya kiislam, funga ya Ashura, aliyoieleza ni funga bora baada ya Ramadhani ambayo Mtume (SAW) aliifunga mara baada ya kuhamia Madina.

Naye Katibu wa sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Sultan Nassor amewahimiza waislam kuendelea kuwa wacha Mungu kwa kumcha Allah (S.W) kwa haki ili kujiepusha na yote aliyoyakataza.

Akizungumza kwenye msikiti huo wa Abuu Ubayda, Fuoni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mahad Istiqama, Sheikh Said Khalfan aliisihi jamiii kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Mufti katika kutatua changamoto zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news