Rais Dkt.Samia awataka wanawake kusimamia maadili ya jamii nchini

ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake kushikamana na kuilea jamii katika malezi yaliyo bora kimaadili ili kuiepusha jamii na vitendo viovu.

Rais Dkt.Samia ametoa tamko hilo leo Julai 16,2023 katika kongamano la wanawake wa Kiislam Zanzibar mwezi 27 katika maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu 1445-Hijjiria lililofanyika ukumbi wa Golden Tulip.

Aidha, Rais Samia amesema kila mwanamke ana wajibu wa kusimamia maadili kwa kuwa ana mchango mkubwa sana katika kujenga au kumomonyoa maadili ya familia na jamii kwa ujumla.

Vile vile, Rais Samia amesema hivi sasa wanawake wamekuwa mstari wa mbele kupigania haki na kushiriki katika masuala ya kitaifa na kijamii kwa kufanya kazi kwa uadilifu, uhakika na weledi mkubwa ambazo awali walidhaniwa hawaziwezi.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka wanawake kujiepusha na vitendo vya unyanyasaji kwa kuwa vinarejesha nyuma maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Rais Samia pia amesema ukosefu wa elimu ya msingi ya dini unaathiri jamii na kusababisha vitendo vinavyokiuka maadili kama udhalilishwaji wa kijinsia, wizi na matumizi ya dawa za kulevya na kuliondoshea taifa heshima, haiba na kuua vizazi vyetu.

Hali kadhalika, Rais Samia amewasihi wanawake kujiendeleza kielimu na kujitokeza kutumia fursa za kimaisha kila zinapojitokeza ili waweze kuinusuru jamii kwa kupambana na changamoto zinazojitokeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news