Jambo kubwa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)

DAR ES SALAAM-Watumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), wamesisitizwa kufanya kazi kwa nidhamu ili kuhakikisha kuwa dira na maono ya taasisi yanafikiwa kama yalivyopangwa katika mpango mkakati mpya wa chuo ulioanza kutekelezwa Julai Mosi, 2023.
Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Elifas Bisanda amesisitiza hilo katika uzinduzi wa maadhimisho ya Juma la Utumishi wa Umma kwa taasisi hii linaloadhimishwa kuanzia Agosti 7, 2023 hadi Agosti 14, 2023.
Watumishi kutoka vituo vya mikoa ya Morogoro, Pwani, Ilala, Kinondoni na makao makuu walikutana kwa pamoja katika uzinduzi huo uliofanyika Makao Makuu ya Chuo Kinondoni jijini Dar es Salaam tarehe 7 Agosti, 2023. Vituo vingine vyote vya OUT nchi nzima vitakutana kikanda kuanzia tarehe 9 Agosti 2023.
“Licha ya kwamba kuajiriwa serikalini kunampa mtumishi uhakika wa mkataba wa muda mrefu, lakini bado tuna wajibu wa kufanya kazi kwa nidhamu ya hali ya juu na bidii na kwa kuzingatia kiapo cha utumishi wa umma ambacho kila mtumishi ameapa,”amesema Prof.Bisanda.
Aliendelea kusisitiza kuwa, kila mtumishi ahakikishe anawajibika kwa kuwatendea haki na kuwapatia huduma bora wageni wote hasa wanafunzi wanaofika katika vituo vya OUT vilivyopo nchi nzima kujisomea, kupata maelekezo na huduma mbalimbali.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. George Oreku amesema, lengo kuu la maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma kwa mwaka huu kwa OUT ni kujadili, kuelewa na kuutekeleza mpango mkakati mpya wa chuo wa mwaka 2023/24 mpaka 2025/26 uliozinduliwa hivi karibuni na umeanza kutekelezwa rasmi.
“Ajenda yetu kuu mwaka huu ni kuzungumzia mpango mkakati mpya, lengo kuu la mpango mkakati huu ni kuleta mabadiliko kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kukipeleka katika kiwango kingine cha juu zaidi. 

"Hivyo kutakuwa na timu maalum ya mpango mkakati itakayokuwa inatoa mafunzo kuhusu malengo ya mpango mkakati huu na mfumo mpya wa upimaji wa utendakazi wa watumishi,”amesema Prof.Oreku.
Akizungumza,Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Huduma za Kitaalam, Prof.Deus Ngaruko amesema, wiki ya utumishi wa umma ikawe chachu kwa watumishi kurudisha ari ya kukitumikia chuo hiki kwani kuendesha chuo ambacho kinatoa elimu ya masafa ni kazi ngumu kutokana na mifumo yake kutokueleweka vyema katika jamii.
“Tangu chuo hiki kimeanzishwa kwa miaka mingi kimekuwa ni chuo bora barani Afrika, tumekuwa chuo namba moja Afrika kwa miaka mingi sana. Kidunia tupo nafasi ya 13 katika vyuo vinavyotoa huduma ya elimu masafa na huria kati ya vyuo 130. 

"Mafanikio yote haya ni kutokana na jitihada kubwa inayofanywa na watumishi na uongozi wa chuo licha ya changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo.”amesema Prof. Ngaruko.

Sambamba nao, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Huduma za Mikoa na Teknolojia za Kujifunzia, Prof. Alex Makulilo amesema, licha ya viongozi na watumishi wanaopangiwa katika vituo vya mikoa kuwa na majukumu mengi amewataka kuendelea kusimama imara kutokana na baadhi ya vituo kukabiliwa na uchache wa watumishi.
“Ni kweli unakuta mtumishi kaajiriwa kada tofauti lakini akifika katika vituo vya mikoa anakutana na majukumu ya ziada. Kwa mfano mtumishi ni mhadhiri na pia anapangiwa kuwa mkurugenzi wa kituo cha mkoa. 

"Majukumu ya ualimu lazima atejeleze na majukumu mapya ya ukurugenzi nayo lazima yaende ipasavyo na hali hii inakwenda hadi kwa watumishi wengine wa kada mbalimbali. 

"Mnachotakiwa ni kuangalia yale mnayotakiwa kuyafanya na kufungamanisha hizo kazi ziweze kwenda sambamba ili malengo ya mpango mkakati wa chuo yaweze kufikiwa,"amebainisha Prof.Makulilo.

Juma la Utumishi wa Umma ni juma maalum kwa watumishi wote wa mashirika ya umma na taasisi zake ambalo huadhimishwa kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya Bara la Afrika.
Kwa OUT, maadhimisho haya yalipaswa kuwa Juni 16 hadi Juni 23, 2023 baada ya kuahirishwa sasa yanaadhimishwa kuanzia Agosti 7, 2023 hadi Agosti 14, 2023 ambapo watumishi kutoka vituo mbalimbali wanakutana kikanda ili kupata mafunzo ya mfumo mpya wa ujazaji wa tathmini za kiutumishi, lakini pia kujuzwa juu ya mpango mkakati mpya wa Chuo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news