Makandarasi wazawa wafundwa

DODOMA-Makandarasi wazawa wametakiwa kuzisimamia kampuni zao kwa ufasaha kwa kufuata sheria za ulipaji wa kodi kwa wakati na kufanya kazi kwa weledi kwa kutumia wataalamu stahiki katika sekta mbalimbali ili kukwepa changamoto katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo Makandarasi wazawa kibiashara, jijini Dodoma, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mha. Rhobin Nkori, alisema kuwa lengo moja wapo la kufanya mafunzo hayo ni pamoja na kutoa elimu kwa makandarasi kuhusiana na mvutano baina yao na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).

“Nimefurahi kuona kwamba moja ya mada itakayofundishwa ni kuhusu masuala ya kodi kwa makandarasi, hii itatusaidia kupunguza matatizo makubwa sana kati ya wakandarasi na TRA,”alisema Msajili.

Aidha, Mha. Nkori, alisema makampuni mengine hutumika kufanya kazi kwa majina ya wamiliki wengine yanayopelekea mvutano pindi kazi inapoenda kukaguliwa na TRA kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi(CRB) hivyo amewataka wamiliki wa makampuni kusimamia vyema makampuni yao ili kuepuka changamoto hizo.

Mha. Nkori amesisitiza kuwa ili kuendelea kujenga taswira nzuri kwa makandarasi nchini, Bodi itaendelea kuwachukulia hatua kisheria makandarasi wote wanaokiuka maadili yao ya kazi.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya SONCO ENGINEERING COMPANY LIMITED, Mha. Baraka Materu, ameiomba serikali kuweka mikakati maalumu ya kuwashirikisha wakandarasi wazawa wakati wa utekelezaji wa miradi mikubwa ili kuwajengea uwezo makandarasi hao kutokana na teknolojia mpya ambayo watajifunza kupitia miradi hiyo.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayotolewa na Bodi hiyo yameshirikisha makandarasi kutoka sehemu mbalimbali nchini lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo makandarasi hao katika mujukumu yao ya kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news