Rais Dkt.Mwinyi aeleza mikakati Sekta ya Maji

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, itaendelea kufanya utafiti utakaoonesha njia bora zaidi za uvunaji wa maji ya mvua.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Afisa wa Maji,Usafi na Mazingira wa UNICEF, Marko Msambazi alipotembelea maonesho kabla ya kulifungua Kongamano la Maji Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar Wilaya ya Mjini Unguja na kulia kwa Rais ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Shaib Hassan Kaduara na Naibu Waziri wa Maji Tanzania, Mhandisi Maryprisca Mahundi.(Picha na Ikulu).

Sambamba na maji kwenye mabwawa ili kutafuta vyanzo vingine vya maji na hatimaye kuongeza ufanisi kwenye sekta ya maji nchini kwa manufaa ya wananchi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Agosti 16,2023 alipofungua Kongamano la Maji kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Verde, Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi.

Dkt.Mwinyi, aliiasa jamii kuendelea kuilinda miundombinu ya maji na kuvilinda vyanzo vya maji vilivyopo kwa kuviepusha na shughuli zao zikiwemo ujenzi na kuanzisha makazi.

Aidha, aliitaka jamii kuendelea kuimarisha mazingira kwa kupanda miti ambayo ni muhimu kwa upatikanaji wa mvua.

Pia, Dkt.Mwinyi aliwaagiza viongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na watafiti wanaofanya utafiti kwenye sekta hiyo, ili wawe na mipango madhubuti ya kukusanya na kutumia matokeo ya utafiti unaofanywa Zanzibar kwa maendeleo ya taifa.

Halikadhalika aliutaka uongozi wa wizara hiyo, kuandaa mpango wa muda mrefu wa Sekta ya Maji ili usaidie kubainisha miongozo ya sekta hiyo na hatimaye kupunguza changamoto zilizopo.

Vilevile, Dkt.Mwinyi aliutaka uongozi wa wizara hiyo kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, kuandaa utaratibu wa kuyatambua na kuyapatia hatimiliki maeneo yote ya vyanzo vya maji Zanzibar.

Alisema, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya maji kwa kutekeleza miradi mikubwa kama ilivyopangwa na kuelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, kufuatia ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Pia, alieleza miradi mikubwa ya maji inayoendelezwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia fedha za Mkopo wa Ahueni ya UVIKO kutoka shirika la Fedha duniani (IMF) itatoa mchango mkubwa na kuondoa changamoto za maji zilizopo kwenye maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Juma Aweso, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Maryprisca Mahundi alieleza Serikali ya SMT kupitia wizara ipo hatua za mwisho za miradi yake mikubwa ya kumtua ndoo ya maji mama kichwani.

Naye, Waziri wa Maji Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara, alieleza nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jitihada zake za kuwafikishia wananchi huduma za maji safi na salama na kueleza mwezi Septemba, mwaka huu Serikali kwa mara ya kwanza inatarajia kuzindua tenki la maji la lita milioni 32, ambalo litasambaza maji kwenye maeneo mengi ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news