Hali ya uchumi yazidi kuimarika, Waziri Mkuu aweka wazi hatua

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo hadi kufikia Julai, 2023 mfumuko wa bei umeendelea kupungua na kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 4.5 ya Julai, 2022.

Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirishwa Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

"Kutokana na jitihada madhubuti na usimamizi wa Serikali, ni matarajio yetu kwamba mfumuko wa bei utaendelea kupungua na kubaki ndani ya lengo, hasa ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa chakula nchini unazidi kuimarika."

Amesema, Tanzania imeendelea kuwa na mfumuko wa bei wa chini ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia, Waziri Mkuu amesema, katika kuhakikisha Serikali inafikia azma ya kutekeleza utoaji wa huduma kwa wananchi na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati, Serikali imeendelea kuongeza maarifa na matumizi ya teknolojia na mifumo ya TEHAMA kwenye ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vyake mbalimbal

Amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilikusanya shilingi bilioni 26,241.8 sawa na asilimia 93.7 ya lengo ikilinganishwa na shilingi bilioni 24,396 mwaka 2021/2022.

"Kati ya kiasi kilichokusanywa, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 21,411.4, sawa na asilimia 95.6 ya lengo, makusanyo yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 3,845.5, sawa na asilimia 83.5 ya lengo na mapato kutoka vyanzo ya halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 984.9, sawa na asilimia 97.3 ya lengo."

Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema, pamoja na jitihada zinazofanyika katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato, bado kuna changamoto kadhaa ikiwemo ubadhirifu kutoka kwa watumishi wasio waaminifu.

Sambamba na kutosomana kwa baadhi ya mifumo na kutokuwa na mifumo imara ya TEHAMA katika baadhi ya taasisi.

Kutokana na changamoto hizo za kusimamia na kuimairisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, Waziri Mkuu amesema, Serikali imeendelea kutekeleza hatua mbalimbali.

"Moja ni uboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini katika sekta za uzalishaji ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi.

"Pili ni kutambua na kusajili biashara zisizo rasmi na zinazoendeshwa kidigitali ili kutanua wigo wa mapato na tatu ni kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kuongeza ulipaji kodi kwa hiari."

Amesema, hatua ya nne ni kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na tano ni kudhibiti misamaha ya kodi ili isizidi asilimia moja ya Pato la Taifa.

Pia, Waziri Mkuu amesema, Serikali iliunda mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ujulikanao kama TAUSI ili kupunguza urasimu uliokuwepo kwenye ukusanyaji wa mapato.

"Mfumo huu mpya ni wa kidijitali na humrahisishia mfanyabiashara kufanya malipo ya halmashauri kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu yake ya kiganjani au kompyuta.

"Mfumo huu umelenga kumsaidia mteja kujihudumia mwenyewe, hali ambayo haimlazimu tena kwenda ofisi za halmashauri kuomba au kulipia tozo, ushuru, leseni, faini au vibali mbalimbali. Badala yake anaweza kufanya mwenyewe kupitia dirisha la mteja au Taxpayer Portal."

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema, Serikali imeweka mikakati kadhaa katika kudhibiti upotevu wa makusanyo ya ndani kwa kutumia mashine za kukusanyia ankara za mapato (PoS).

Ili kufikia azma hiyo, amesema Serikali ilisimika mfumo ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya katika halmashauri zote nchini unaojulikana kama TAUSI.

"Niwakumbushe watumishi wa umma kuwa bado tunalo jukumu la kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan alivyosisitiza juu ya usimamizi wa ukusanyaji mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati akifunga mafunzo ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa mjini Kibaha.

"Katika hili nawaelekeza wataalamu wetu wa ndani wa mifumo na TEHAMA, wabuni programu tumizi ya kuweza kutambua risiti halali na zisizo halali ili kuweza kujihakikishia kuwa mapato yote yanayokusanywa yanaingia serikalini.

"Vilevile, waweke utaratibu wa kufanya kaguzi za kushtukiza kwenye mashine za PoS ili kubaini kama kuna ukiukwaji wowote unaofanyika sambamba na kuwa na utaratibu endelevu wa ufuatiliaji na mfumo wa usalama maalum wa utunzaji taarifa (back-up)."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news