OSHA imefanya makubwa zaidi-Waziri Mkuu

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema mbali na kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini, Serikali imeendelea kutekeleza azma yake ya kujenga mazingira bora ya kazi na wafanyakazi.

Vilevile, imeendelea kuhakikisha wafanyakazi wanapata stahili zao, vitendea kazi, kufuatilia kwa karibu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi.

"Hii, ni kutokana na ukweli kwamba masuala ya afya na usalama kazini ni haki ya msingi ya mfanyakazi na yanapaswa kusimamiwa kikamilifu;

Ameyasema hayo leo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirishwa Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

"Nitumie fursa hii kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kusimamia masuala ya afya na usalama mahali pa kazi kupitia taasisi ya OSHA ambayo ina jukumu hilo kisheria."

Amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, OSHA imefanya ukaguzi katika maeneo ya kazi 20,067.
 
Ukaguzi huo ni wa usalama wa umeme, mitambo ya kuzalishia mvuke, mitungi ya gesi na hewa, majengo na majenzi, egonomia, zana za kunyanyulia vitu vizito na vipimo vya ubora wa mazingira ya kazi.

"Sambamba na kaguzi hizo, OSHA imewezesha maeneo ya kazi kusimika mifumo ya kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokana na mazingira ya kazi."

Pia, Waziri Mkuu amesema, OSHA imesajili maeneo ya kazi 11,036 na kuhamasisha wafanyakazi kupima afya zao kulingana na vihatarishi vilivyomo kwenye kazi wanazozifanya, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi.

Sambamba na kusimamia viwango vya kazi pamoja na masuala ya afya na usalama mahali pa kazi. Lengo ni kuhakikisha Sheria ya Usalama mahali pa kazi inatekelezwa ipasavyo.

"Ninayofuraha kulieleza Bunge lako tukufu kuwa kutokana na mafanikio ya OSHA, nchi mbalimbali zimekuwa zikija kujifunza kutoka kwetu.

"Baadhi ya nchi hizo ni Zimbabwe, Botswana na Kenya. Aidha, hivi karibuni tumepokea maombi ya ugeni kutoka Eswatini na Afrika Kusini watakaokuja kujifunza kutoka kwetu masuala mbalimbali ikiwemo Mfumo wa TEHAMA wa Usimamizi wa Taarifa za Kaguzi nchini (Workplace Inspection Management System - WIMS).

"Aidha, ni jambo la kujivunia pia kuona mtaalamu wetu kutoka OSHA ndiye anayesimamia Dawati la Masuala ya Afya na Usalama mahali pa Kazi katika Ofisi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zilizopo Gaborone nchini Botswana. Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu."

Waziri Mkuu amesema Agosti 7, 2023 alipata fursa ya kuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kugawa vitendea kazi na magari 30 ambapo magari 17 ni ya ofisi za mikoa za Idara ya Kazi na 13 ni ya OSHA.

Magari hayo na vifaa vya kupima afya na usalama mahali pa kazi, Waziri Mkuu amesema vilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 4.3 na vilitolewa ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa ofisi hizo.

Amesema, magari hayo 30 yalinunuliwa kwa fedha za ndani ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozitoa katika maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi, 2023 zilizofanyika kitaifa mkoani Morogoro.

"Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi yake ndani ya kipindi kifupi sana.

"Na nisisitize watendaji wote kuongeza ufanisi katika utendaji wa kila siku pamoja na kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Usalama na afya mahali pa kazi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news