Ulipaji wa fidia kupitia WCF waongezeka

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema,ulipaji wa fidia kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeongezeka.

Ni kutoka shilingi bilioni 13.19 zilizolipwa kwa mwaka katika kipindi kilichoishia Juni, 2021 na kufikia shilingi bilioni 17.93 kwa mwaka katika kipindi kilichoishia Juni, 2023.

Ameyasema hayo leo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirishwa Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

"Ongezeko hili linaufanya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuwa umelipa jumla ya shilingi bilioni 62.04 kwa wanufaika 11,587 tangu ulipoanza kulipa fidia Julai, 2016 hadi ilipofika Juni, 2023."

Amesema, WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263 kwa lengo la kulipa fidia wafanyakazi wanapopata ulemavu au kufariki kutokana na magonjwa au ajali zitokanazo na kazi.

"Kama yalivyo madhumini ya kuanzishwa kwake, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi umeendelea kutekeleza kwa ufanisi jukumu la kulipa fidia kwa wafanyakazi waliopata ajali ama magonjwa yanayotokana na kazi.

"Aidha,mfuko unalipa fidia kwa wategemezi wao pale ambapo mfanyakazi anafariki kutokana na ajali ya kikazi,"amefafanua Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema, pamoja na malipo haya, tathmini ya uhai na uendelevu wa Mfuko iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani kwa kipindi cha kuishia Juni 30, 2022 imeonesha kuwa mfuko ni endelevu na uko imara.

Aidha, kwa mujibu wa hesabu ambazo zimewasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya ukaguzi hadi kufikia Juni 30,2023, Waziri Mkuu amesema, thamani ya mfuko imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 665.06.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news