Norway yatoa fungu miradi ya mabadiliko ya tabianchi

DAR ES SALAAM-Serikali ya Tanzania imenufaika na shilingi bilioni 7.3 kutoka Serikali ya Norway kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na inayotekelezwa nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim wakisaini makubaliano ya ushirikiani kati ya Serikali ya Tanzania na Norway kuhusu ushirikiano katika hifadhi ya mazingira jijini Dar es Salaam, Septemba 7, 2023. Aneyeshuhudia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo.

Hayo yamejiri baada ya Serikali hizo mbili kusaini makubaliano ya kushirikiana Septemba 7, 2023 katika shughuli za mazingira, hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania itajengewa uwezo katika utekelezaji wa shughuli za mazingira.

Alisema makubaliano hayo ni chachu katika kuijengea Tanzania kuweza kunuifaika na fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutoka nchi zilizoendelea ambazo ziliahidi.

Pia, alisema Norway imeiunga mkono Tanzania katika mikakati yake ikiwemo kupunguza gesi joto, utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032 pamoja Sera ya Uchumi wa Bluu.

“Makubaliano tuliyosaini leo yatasaidia katika miradi yetu ya kimazingira katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji, afya na ardhi na tuishukuru sana Serikali ya Norway, na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tunafurahi sana kwa miradi hii ambayo inakwenda kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dkt. Jafo.

Kwa upande wake Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim aliyesaini kwa niaba ya Serikali ya Norway alisema kuwa makubaliano hayo ni matunda ya uhusiano wa muda mrefu wa Serikali hizo mbili.

Alisema nchi yake imejipanga katika kuyatendea haki makubaliano hayo kwa kuelekeza miradi hiyo kwa wananchi wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yao.

Mhe. Anne alisema kuwa Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kufanya utafiti kwa ajili ya katika kuimarisha usimamizi wa Biashara ya Kaboni ambayo imeshika kasi hapa nchini.

Naye Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Maendeleo (UNFCC) Bw. Peter Malika alisema fedha hizo zilizotolewa zitasambazwa katika wilaya sita za Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kusaidai katika miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema pia kutakuwa na mafunzo kwa jamii zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi kuhusu namna ya kutambua changamoto hizo kwa ajili ya mikakati ya kuanzisha miradi.

Aprili 21, 2008 nchi hizo mbili zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi hatua iliyoanzisha Kituo cha Taifa Kufuatilia Kaboni (NCMC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news