Timu za Tanzania zampa tabasamu Waziri Mkuu michuano mbalimbali

NA GODFREY NNKO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema, Tanzania imeendelea kupiga hatua kubwa katika sekta ya michezo ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyasema hayo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirishwa Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

"Kwa upande wa michezo, nchi yetu imeendelea kupata mafanikio makubwa. Sote tumeshuhudia vilabu vyetu viking’ara katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

"Hivi karibuni tumeshuhudia Timu ya Taifa ya Wasichana Chini ya Miaka 18 (U18) ikichukua ubingwa wa mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) baada ya kuishinda Timu ya Uganda kwa bao moja bila katika mchezo uliofanyika kwenye Viwanja vya Azam jijini Dar es Salaam."

Pia, Waziri Mkuu ameipongeza JKT Queens ambayo imefanikiwa kuchukua ubingwa wa CECAFA na hivyo kupata fursa ya kuwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika Mashindano ya Vilabu ya Afrika.

"Ushindi wa timu hizi za mpira wa miguu za wanawake ni wa kujivunia sana. Nyote mtakubaliana nami kuwa timu za wanawake zimehamasika na zinaendelea kushindana kwa kasi ya juu mno.

"Ninawatakia kila la heri JKT Queens katika mashindano yanayofuata na nitoe wito kwa wapenzi wa michezo na Watanzania wote kwa ujumla tuendelee kuwaunga mkono ili wazidi kupeperusha bendera ya nchi yetu. Niwasihi waendelee kujifua kwani ushindi ni lazima."

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameipongeza Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ambayo katika mashindano ya Afrika (Africa Games) imeshika nafasi ya tatu na kupata medali ya shaba. "Hongereni sana."

Kwa upande wa mchezo wa ngumi maarufu masumbwi, Waziri Mkuu amewapongeza wanamasumbwi walioshiriki katika mashindano mbalimbali.

"Kipekee nimpongeze Grace Mwakamele aliyetunukiwa medali ya fedha katika mashindano ya ngumi yaliyofanyika Yaounde nchini Cameroon, huyu ni mwanamke wa kwanza Mtanzania kushinda medali ya kimataifa.

"Pia, ninampongeza bondia Yusuph Changarawe aliyetunukiwa medali ya shaba katika mashindano hayo yaliyofanyika tarehe 25 Julai hadi tarehe 6 Agosti.

"Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitoishukuru Serikali ya India kupitia Ubalozi wake hapa nchini pamoja na Taasisi ya Kalamandalam kwa kuwaunga mkono wachezaji wetu kwani kwa miaka miwili mfululizo wamekuwa wakiandaa hafla maalum ya kuwapongeza na kuwapa zawadi washindi wetu."

Aidha, kufuatia mashindano ya Africa Open katika mchezo wa Golf yaliyofanyika nchini Ghana, Waziri Mkuu amesema, mchezaji mwanadada shupavu Madina Iddi ameibuka bingwa wa mashindano hayo.

"Nitumie fursa hii kumpa pongezi nyingi sana kwa ushindi huo mkubwa. Vilevile, niwapongeze wanawake wote wanaothubutu kushiriki katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi. Jitihada zenu tunaziona na kwa hakika mmeendelea kuliheshimisha sana Taifa letu."

Katika michuano ya Klabu Bingwa na Shirikisho Barani Afrika, Waziri Mkuu amezipongeza timu za Yanga, Simba na Singida Fountain Gate kwa kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya pili ya michuano hiyo.

"Hakika mmeanza vema. Nitumie fursa hii kuwatakia kila la heri katika mashindano yanayoendelea, mpate ushindi mnono na kuweza kuingia hatua ya makundi ili kuzidi kutupa raha Watanzania.

"Kipekee, niipongeze timu ya Simba ambayo imekuwa miongoni mwa vilabu nane bora barani Afrika ambavyo vitashiriki michuano ya African Football League.

"Michuano hiyo inatarajia kuzinduliwa mwezi Oktoba 2023 jijini Dar es Salaam. Nawasihi Watanzania kujitokeza kwenye ufunguzi wa michuano hiyo kwani inaitangaza Tanzania kimataifa. Hongera sana."

Mbali na hayo, Waziri Mkuu amesema, timu yetu ya Taifa au Taifa Stars jana ilishiriki katika mechi ya michuano ya kufuzu kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika (Africa Cup of Nations 2024) yatakayofanyika nchini Ivory Coast.

Waziri Mkuu amesema, katika michuano hiyo Tanzania ilihitaji kushinda au kutoka sare ili kuweza kufuzu katika kundi lake.

"Ninayo furaha sana kuipongeza Taifa Stars kufuzu michuano ya kuwania kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kupambana na Timu ya Taifa ya Algeria huko nchini Algeria.

"Katika mechi hiyo timu yetu ilitoka suluhu (bilabila) na kuifanya ipate tiketi ya kuendelea na mashindano hayo. Ninaipongeza sana timu yetu ya Taifa na kuitakia kila la heri katika mashindano yajayo.

"Nami nitumie fursa hii kuwasihi Watanzania wenzangu tuendelee kuwaunga mkono ili wapate hamasa zaidi na kutuletea ushindi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news