Waziri Mkuu atoa maagizo nane yanayogusa watumishi wa umma

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametoa maelekezo mahususi nane ambayo yanagusa wafanyakazi na watumishi wa umma nchini.

Ameyasema hayo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirishwa Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

Mosi, Waziri Mkuu amewataka waajiri wachukue hatua za kuimarisha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi wao dhidi ya vihatarishi vilivyomo katika maeneo yao ya kazi.

Waziri Mkuu amesema, hatua hizo ni pamoja na kuwa na mwongozo wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kufanya tathmini ya vihatarishi mahali pa kazi.

Pia, kuhakikisha wafanyakazi wao wanapimwa afya ili kubaini athari ya vihatarishi kwa mfanyakazi na kuhakikisha maeneo yao yanafanyiwa kaguzi za usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi na kulinda uwekezaji wao.

"Aidha, nitoe wito kwa watumishi wa OSHA wawe waadilifu wanapoendesha mazoezi ya ukaguzi mahali pa kazi na kuchukua vipimo vya wafanyakazi."

Pili, Waziri Mkuu amewataka wafanyakazi kuhakikisha wanazingatia taratibu na miongozo ya kujilinda dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali au magonjwa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.

Amesema, hatua hiyo itasaidia kulinda afya na usalama wao pamoja na kumpunguzia mwajiri gharama za uendeshaji pale wanapougua au kupata ajali wakiwa kazini.

Tatu, Waziri Mkuu ameutaka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uongeze wigo wa kutoa elimu kwa wafanyakazi ili watambue huduma zinazotolewa na mfuko huo.

Vilevile, waajiri watumie ipasavyo mifumo ya TEHAMA kupata huduma, kujisajili na kuwasilisha kwa wakati michango katika mfuko huo.

"Nne, nipende kuwasisitiza wafanyabiashara na watoa huduma watoe risiti halali kupitia mashine za kielektroniki (EFDs) wakati wa mauziano ya bidhaa au utoaji wa huduma kwa wateja.

Kwa upande wa wateja, niwakumbushe kuwa ni wajibu wao kudai risiti yenye thamani halisi ya fedha walizotoa.Tano, Maafisa Masuuli waimarishe usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024."

Sita, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Serikali, waimarishe ukusanyaji wa mapato na kufanya matumizi kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele vilivyoainishwa katika bajeti sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato.

Aidha, saba, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma watenge muda wa kwenda kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.

"Wafuateni, wasikilizeni na kutatua kero zao ili wasipoteze muda mwingi kufuatilia, lakini pia wasilazimike kwenda ngazi za juu au kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa kwa masuala ambayo mngeweza kuyafanyia kazi."

Nane, Waziri Mkuu amesema, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watumishi wote wanaosababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

"Nawaelekeza wakuu wa mikoa yote kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuwabaini wabadhirifu hao, kuwachukulia hatua mara moja na kutoa taarifa kwa mamlaka,"ameagiza Waziri Mkuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news