Mauzo ghafi ya bima yafikia trilioni 1.2/- nchini

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA),Dkt.Baghayo A.Saqware amesema, Sekta ya Bima nchini imekua kwa wastani wa asilimia 12.8 kwa mwaka.

Dkt.Saqware amesema, kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka shilingi bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia takribani shilingi trilioni 1.2 mwaka 2022.

Ameyasema hayo leo Septemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Kupitia vikao kazi hivyo,TIRA ni taasisi ya 15 kati ya mashirika na taasisi za umma zilizopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina dhidi ya wahariri wa vyombo vya habari hapa nchini.

Lengo la vikao hivyo ni kuelezea majukumu na mafanikio waliyoyapata ili umma uweze kufahamu kwa kina kuhusiana na yale ambayo yanaendelea katika mashirika na taasisi hizo ambao ndiyo wamiliki.

Pia, Kamishna huyo amesema,mchango wa Sekta ya Bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68 kwa mwaka 2021.

“Mamlaka imeendelea kuongeza gawio serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 mamlaka imeweza kulipa gawio kwa Serikali la jumla ya shilingi bilioni 2.9.”

Sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022, Dkt.Saqware amesema, sekta hiyo imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173 nchini.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), chini ya Sheria ya Bima Na.10 ya mwaka 2009, ni taasisi ya Serikali ilioanzishwa ili kutekeleza majukumu ya kusimamia soko na kuendeleza biashara ya bima nchini na masuala yanayohusiana na bima kwa mujibu wa sheria ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa majukumu ya TIRA ni kusajili kampuni za bima nchini, kusimamia na kukagua mwenendo wa kampuni za bima nchini.

“Nichukue fursa hii kuishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kutoa nafasi kwa taasisi na mashirika ya umma kuongea na wahariri wa vyombo vya habari ili kupitia kwao waweze kujulisha umma kile ambacho tunakifanya.”

Pia,kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya huduma za bima, kutoa elimu ya bima kwa umma na kusimamia biashara ya bima na masuala yanayohusika na bima kwa mujibu wa sheria.

Wakati huo huo, Dkt.Saqware amesema, wamekuwa wakiishauri Serikali kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo bima nchini, ikizingatiwa kuwa hii ni tasisi ya Muungano ikiwa inasimamiwa na Bodi ya Taifa ya Bima.

Dkt.Saqware amesema, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima ni taasisi ya Muungano chini ya Wizara ya Fedha na inaongozwa na Kamishna wa Bima akisaidiwa na Naibu Kamishna na inasimamiwa na Bodi ya Taifa ya Bima inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi.

Amesema,Muundo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) uliidhinishwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 11 Septemba 2021.

Kamishna huyo amesema, muundo ulioidhinishwa unajumuisha Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO), Kurugenzi tatu, Ofisi ya Zanzibar, Ofisi za Kanda na vitengo saba.

“Sisi katika katika kutekeleza majukumu yetu na kusogeza huduma kwa wananchi tuna ofisi makao makuu Dodoma, Zanzibar, Dar es Salaam.”

Pia, amesema wana ofisi za kanda mkoani Tabora ambayo inahudumia Mkoa wa Tabora, Katavi na Kigoma.

Kwa upande wa ofisi ya Kanda ya Mashariki iliyopo Dar es Salaam amesema, inahudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Dkt.Saqware amesema, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ofisi ipo mkoani Mbeya ambayo inahudumia mikoa ya Mbeya, Njombe, Rukwa, Iringa na Songwe.

Aidha, Kanda ya Ziwa ofisi ya TIRA ipo jijini Mwanza ikiwa inahdumia mikoa ya Mwanza,Mara, Shinyanga, Kagera, Simiyu na Geita.

Kanda ya Kaskazini, Dkt.Saqware amesema, ofisi ipo mkoani Arusha ikiwa inahudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Vile vile, Kanda ya Kati ofisi ipo mkoani Dodoma ikihudumia mikoa ya Dodoma, Manyara na Singida. Kwa upande wa Kanda ya Kusini ofisi ipo mkoani Lindi ikihudumia mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Amesema,mamlaka imefanikiwa kusajili watoa huduma 1361 hadi Septemba 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Wakati huo huo, Dkt.Saqware amezishauri taasisi za umma na sekta binafsi nchini kutumia huduma za bima nchini ili waweze kujiongezea kipato na kuondokana na umaskini.

“Kwa hiyo ninawasihi taasisi za umma pamoja na watu binafsi kutumia huduma za bima nchini ili kujiongezea kipato na kujiondolea umaskini.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news