Zanzibar kuendelea kusimamia mila, silka na tamaduni

ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia mila, silka na tamaduni za Kizanzibari ili Zanzibar izidi kusifika kwa maadili mema.
Alhajj Hemed ameyasema hayo wakati akiwasalimia waumini wa Mskiti wa Ijumaa Malindi Jongeani alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema ni wajibu wa wananchi kusimamia Maadili mema yaliyoipatia sifa Zanzibar na kuacha kuiga Maadilli ya Mataifa mengine ambayo yanakwenda kinyume na urithi wa Utamaduni wa Mzanzibari.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali ili kusimamia Maadili na kusaidia kuondoa Mmong'onyoko wa Maadili na vitendo viovu vinavyoendelea katika Jamii.

Mhe. Hemed amesema wakati umefika wazanzibari kuungana katika malezi ya watoto kwa kuzingatia miongozo ya Qur-an na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) ili kupata watoto watakaoleleka katika maadili mema watakaosaidia kuleta maendeleo nchini kwa kuwa na hofu juu ya Allah (S.W)

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewasisitiza waumini hao na wananchi kwa ujumla kuiunga Mkono Serikali katika kudumisha Amani na Utulivu ili kutka fursa kwa Serikali kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Akitoa Khutba katika Sala hiyo ya Ijumaa Ustadh Said Abubakar Said Al Abbasy amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuiombea Dua nchi ya Morocco ambayo imekumbwa na tetemeko la Ardhi na kuwakumbusha kuwa mtihan huo ni mazingatio kwa kila Muumini kujikaribisha na Allah Mtukufu.

Amesema miongoni mwa dalili za kiama ni kutokea kwa mtetemeko wa ardhi, kufa kwa walimu na wanazuoni, kukithiri kwa fitna na kutokea kwa machafuko duniani hivyo, ni vyema kuzidisha Ibada na Dua ili kupata mwisho mwema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news