BoT yawapa darasa watoa huduma ndogo za fedha mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, zaidi ya leseni 1,550 zimetolewa kwa watoa huduma ndogo za fedha walioomba leseni hizo kutoka benki hiyo kuanzia mwaka 2020 hadi sasa huku maombi ya leseni yaliyowasilishwa yakiwa ni 2,050.

Pia,BoT imewataka Watanzania kutambua kuwa haitoi leseni kwa kuangalia umaarufu wa mtu, au ukubwa wa kampuni bali kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu na leseni hutolewa kwa wamiliki na wakurugenzi kudhibiti leseni feki hivyo waombaji wanapaswa kufuata taratibu.

Hayo yamebainishwa Oktoba 6, 2023 na Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka BoT,Deograthias Mnyamani wakati akitoa semina kwa watoa huduma ndogo za fedha wa Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa MCC uliopo Mjini Musoma.

Hatua hiyo ni kufuatia ombi la Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Said Mtanda kumuomba Gavana wa BoT alete wataalamu watoe elimu kwa watoa huduma hao, kwani wengi wao hawana uelewa.

Mnyamani amesema kuwa, upatikanaji wa leseni sio mgumu kama ambavyo baadhi wamekuwa wakidhani. Bali inahitaji umakini na ufuatiliaji kupata leseni na kama maombi yamekamilika mwombaji atapata leseni kuanzia siku 45 hadi siku 60 na sio siku tatu au wiki moja kama ambavyo baadhi wamekuwa wakitapeliwa.

Ameongeza kuwa, Watanzania hawapaswi kuchukua fedha katika taasisi ambazo hazijapewa leseni kutoka BoT na kwamba benki hiyo inaelekea kwenye utoaji wa elimu kwa umma ili kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wahariri, mahakimu, makundi mbalimbali na jamii kwa ujumla ili kuwapa uelewa.

Amesema, gharama za maombi ya leseni kwa upande wa kampuni ni shilingi 500,000, ambazo mwombaji hupaswa kulipia benki.

Amesema, mwombaji wa leseni upande wa kampuni anapaswa kuwa na kampuni iliyosajiliwa BRELA,neno la biashara, awe amelipa ada ya maombi ya kupata leseni, awe na mtaji usiopungua shilingi milioni 20 katika akaunti yake, awe na sera ya ukopeshaji na barua ya maombi

Pia, awe na uthibitisho wa malipo ya fedha iliyotolewa kulipia leseni maombi ya leseni,nakala ya vyeti vya wajumbe vilivyothibitishwa na Mwanasheria na Tini ya Kampuni.

Aidha, awe na Tamko la Fedha inayokopeshwa haihusiani na jinai liwe limegongwa mhuri na Mwanasheria, uraia wa Wajumbe wa bodi, Dodoso lililojazwa kikamilifu katika kanuni,nakala iliyothibitishwa ya cheti cha usajili wa kampuni, maazimio ya bodi yaliyoadhimia kuomba leseni na nakala zilizothibitishwa za hati safi ya kodi.Kwa upande wa mtu binafsi amesema, ada ya maombi ya leseni ni shilingi 300,000, awe na mtaji wa shilingi milioni 20 katika akaunti yake, awe na sera ya ukopeshaji, barua ya maombi, uthibitisho wa kulipa ada,nakala ya vyeti vya taaluma vya wataalamu.

Pia,nakala ya fedha iliyokaguliwa kabla, TIN namba ya biashara,tamko la fedha unayokopesha haitokani na jinai, uthibitisho wa uraia,dodoso lililojazwa kikamilifu,nakala iliyothibitishwa ya cheti cha biashara, taarifa ya kumbukumbu za mikopo na nakala ya annul report.

Amesema, mikoa inayoongozwa kwa kuwa na watoa huduma wengi wa biashara hiyo ni Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Mkoa wa Mara unashika nafasi ya saba. Na amewataka watoa huduma hiyo Mkoa wa Mara kuwa na umoja wao ili kupata suluhisho la kero zao.

Kwa upande wake Amri Mbalilaki, Kaimu Meneja Kitengo cha Uchunguzi kutoka Benki Kuu ya Tanzania amewataka watoa huduma ndogo za fedha ambao wanataka kuanza kufanya biashara hiyo, kufuata sheria kwa kuomba leseni kwanza ili kuwawezesha kufanya biashara hiyo kwa uhakika na kwa mujibu wa sheria.

"Muda wa neema umekwisha, kufanya biashara hii bila leseni ya Benki Kuu ni kosa kisheria na pia kuingia kwenye biashara hii bila kutambua kanuni ni kupoteza, lazima kanuni mtu azitambue afanye biashara kwa ufanisi, BoT ilishatoa muda wa miaka mitatu umeshapita na kisheria ulikuwa mwaka mmoja tu huu ulikuwa muda wa neema,"amesema Amri.

Washiriki wa semina hiyo wameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kutoa elimu hiyo pamoja na kuwa na utaratibu mzuri wa utoaji leseni kwa wafanyabiashara hatua ambayo inachangia ufanisi. Huku wakiomba zaidi elimu hiyo itolewe mara kwa mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news