TARURA kazini, Mhandisi Seff atoa maagizo kwa Mkandarasi barabara ya Kasulu hadi Muyama

KIGOMA-Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff amemwelekeza Mkandarasi Salum Motors Transport Co.Ltd kuhakikisha anakamilisha kwa wakati ujenzi wa barabara ya Kasulu- Kabanga-Kasumo-Muyama kilomita 36 ambapo awamu ya kwanza ya kilomita 12.5 inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Akiwa katika ukaguzi wa barabara hiyo, Mhandisi Seff ameeleza kuwa maagizo yaliyotolewa kwa Mkandarasi hapo awali yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa na kwamba hatarajii suala la maombi ya nyongeza ya muda.
"Leo nimekagua barabara hii kwa mkataba huu wa awamu ya kwanza km 12.5, kazi inaendelea na Mkandarasi anatakiwa kumaliza kazi hii ndani ya muda uliopangwa, kwa maana hiyo sitarajii kuona maombi ya nyongeza ya muda kwani hakuna sababu yoyote ya kufanya hivyo,"amesema Mhandisi Seff.
Kwa upande wake Bi. Naomi Kiogoma mkazi wa Kijiji cha Kasumo amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni mkombozi kwa wakazi wa vijiji hivyo kwani barabara ikikamilika wananchi wataweza kusafirisha mazao kwa urahisi kwenda Kasulu.

"Barabara hii itatusaidia hasa kukuza uchumi wetu, sisi akina mama sasa tutaweza kufanya biashara maana hata kama mtu anataka kuuza mazao kama maharage itakua rahisi kuyafikisha Kasulu," amesema Bi. Naomi.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 36 inajengwa kwa awamu ya kwanza kilomita 12.5 kwa kiwango cha lami na inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 ambapo itagharimu shilingi Bilioni 16.7

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news