Israel yawapa raia wa Gaza saa sita kuhamia Kusini

GAZA-Jeshi la Israel limewapa raia wa Gaza muda wa saa sita kuhamia Kusini katika mitaa maalum.Kwa mujibu wa CNN, haijulikani ni kwa kiasi gani ujumbe huo umepokelewa huku kukiwa na changamoto ya kukatika kwa umeme na mtandao.

Kwa sasa Gaza imekuwa chini ya mashambulizi ya anga kutoka kwa Israel baada ya shambulio la Hamas ndani ya Israel.(Picha na Said Khatib/AFP).

Agizo hilo linakuja kwa wakaazi wa Gaza ikiwa ni siku moja baada ya onyo kutolewa kwa watu milioni 1.1 wanaoishi Kaskazini mwa Gaza kuhama makazi yao.

Vile vile,inaonesha kuwa,kuna ishara kwamba Israel iko tayari kuongeza mashambulizi yake ya kulipiza kisasi dhidi ya Hamas kufuatia mashambulio ya kigaidi ya Oktoba 7, mwaka huu ya kundi hilo na kuua watu 1,300.

Agizo la kuwahamisha liliwafanya makumi ya maelfu ya watu kuondoka makwao huko Gaza Ijumaa, kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Kibinadamu.

Mgogoro wa kibinadamu wa Gaza unazidi kuongezeka huku watu wakionya kuwa wako katika hatari ya njaa. Takribani watu 1,900 wameuawa huko Gaza, kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina.

Awali, kundi la Hamas lililofanya shambulio la kushtusha na la kikatili takribani wiki moja iliyopita, limewataka wakaazi wa Gaza kupuuza amri hiyo ya kuondoka kuelekea Kusini mwa ukanda huo na kuitaja kuwa vita vya kisaikolojia.

Amri ya Jeshi la Israel inayoulenga mji wa Gaza ambao ni makaazi ya maelfu ya raia na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada imesababisha mkanganyiko kwa watu hao ambao tayari wanaukimbia mji huo kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel. Hadi sasa ukanda huo uliozingirwa hauna huduma muhimu za kijamii ikiwemo umeme.

Hata hivyo, agizo hilo linachukuliwa kama ishara nyingine ya mashambulizi ya ardhini yanayotarajiwa ingawa Israel bado haijatangaza uamuzi huo. (Agencies)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news