Prof.Muhongo:Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa, Watanzania wana wajibu wa kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuthamini na kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo.

Sambamba na kwenye viwanda vya zana za kilimo, kwani dhamira yake ilikuwa ni kuona sekta hiyo inachangia kuboresha uchumi na ustawi wa Taifa.

Picha na Mtandao.
 
Hayo yamebainishwa na Mbunge huyo kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi yake Oktoba 14, 2023. Ambapo taarifa hiyo imeeleza kuwa Oktoba 14, 2023, inatukumbusha mengi ambayo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitufanyia kwa lengo kuu la kuboresha uchumi na ustawi mzuri wa Taifa letu.


"Baba wa Taifa alithamini sana kilimo na kuwekeza kwenye viwanda vya zana za kilimo (k.m. UFI), kiwanda cha mbolea, viwanda vya kutumia mazao yetu ya kilimo na ufugaji, vyuo vya kuzalisha wataalamu wa kilimo wa ngazi mbalimbali, vyama vya ushirika, ushirikiano na nchi za nje kwenye sekta ya kilimo, JKT yenye mashamba ya kilimo, tuzo na sherehe za wakulima,"imeeleza taarifa hiyo na kusema.

"Baba wa Taifa alipeleka nje ya nchi vijana wa ki-Tanzania kusomea masuala mbalimbali ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

"Vilevile, Baba wa Taifa aliamua kuwekeza kwenye kilimo kikubwa cha umwagiliaji na moja ya miradi hiyo ni ule wa Bonde la Bugwema la Musoma Vijijini."

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa, "Serikali imeamua kufufua Mradi wa Bugwema ambao miundombinu ya umwagiliaji ilianza kujengwa mwaka 1974. Mradi ukasimama,"

Prof. Muhongo amesema, "nimeomba wizarani kitakuwa ni kilimo cha wakulima wadogo wadogo wanaoishi humo, wenyeji wa hapo na hakuna atakayehamishwa wala kunyang'anywa ardhi kwani ndio makubaliano yangu na Serikali kupitia Wizara ya kilimo pamoja na wakulima wakubwa watakaoletwa." amesema Prof. Muhongo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Musoma Vijijini, Denis Ekwabi amesema kuwa, hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na dhamira njema ya Serikali kuhakikisha kwamba bonde hilo linawanufaisha wananchi wa kijiji hicho cha Bugwema na Mkoa wa Mara kiujumla kiuchumi kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Nao wananchi wa Bugwema, wameishukuru Serikali kwa kuanzisha mchakato wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo wamesema badala ya kufanya Kilimo cha kutegemea mvua, watafanya kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula kwa uhakika na kuwa na ziada ambayo itaweza kusaidia maeneo mengine na hivyo kukuza uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news