TARURA kuanza ujenzi wa Daraja la Mfisi huko Mikumi

MOROGORO-Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani Kilosa imedhamiria kumaliza kero ya muda mrefu ya kukatika kwa mawasiliano katika Kata tatu za Kisanga, Ulaya na Mikumi baada ya kukamilisha taratibu zote za ujenzi wa daraja la Mfilisi litakalokuwa na urefu wa mita 21.75.

Akiongea katika hafla ya kukabidhi rasmi kazi hiyo kwa Mkandarasi ili aanze ujenzi, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa Mhandisi Harold Sawaki amesema kuwa eneo hilo limekuwa changamoto kubwa hasa kipindi cha masika ambapo watu hushindwa kuvuka upande wa pili.

"Mto unapojaa maji mawasiliano hukatika maana kalvati lililopo ni dogo na sasa Serikali imekuja na suluhisho la kudumu la tatizo hili,"amesema Meneja huyo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kasi yake ya kusukuma maendeleo Vijijini kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za miradi.

"Daraja hili linakuja kufungua uchumi wa wananchi na Mhe. Rais anaendelea kuleta fedha nyingi kila eneo iwe barabara, afya, elimu na maeneo mengine na wananchi nyie ni mashahidi wa hili,"amesema Mhe. Shaka.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Dennis Londo amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kutatua kero za wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja katika jimbo la Mikumi.

Akiongea kwa niaba ya wananchi Bi Rehema Mlingwa ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ibegezi amesema kuwa kipindi cha masika eneo hilo huwa linasumbua maana watu hushindwa kuvuka na hata kuvusha mazao yao na kwamba ujenzi wa Daraja hilo ni mkombozi kwao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news