TAWIRI yatakiwa kuwa wabunifu katika utendaji kazi

NA HAPPINESS SHAYO

TAASISI ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imetakiwa kuwa bunifu katika utekelezaji wa majukumu yake ya Utafiti wa Wanyamapori.

Hayo yamesemwa Oktoba 28,2023 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) alipokuwa akizungumza na Menejimenti na watumishi wa TAWIRI katika Makao Makuu ya Ofisi ya TAWIRI jijini Arusha.

"Lazima mchape kazi, muwe wabunifu na muendelee kujifunza kwa wengine na kushirikiana na taasisi zingine zinazofanya kazi zinazofanana na sisi ziwe za kitaaluma, vyuo vikuu na zinginezo," Mhe. Kairuki amesisitiza.

Katika kutekeleza agizo hilo, Mhe. Kairuki ameitaka taasisi hiyo kujitangaza ndani na nje ya nchi na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi mbalimbali ili kuiongezea Serikali mapato.

"Muendelee kuzitangaza tafiti zenu kimataifa ili zitumike pia katika mataifa kwenye maeneo mengine," Mhe. Kairuki amefafanua.

Aidha, amewataka kutafuta vyanzo vingine vya mapato kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuiinua taasisi hiyo.

Kuhusu utalii, Mhe. Kairuki amewaelekeza watafiti hao kufanya tafiti za kiutalii na kutoa mapendekezo ya mazao mapya ya utalii ili kuikuza Sekta hiyo.

"Niwapongeze kwa zao jipya la Utalii wa Kiutafiti lakini muendelee kufanya tafiti ya mazao mapya ya Utalii,"Mhe. Kairuki amesema.

Kuhusu ustawi wa watumishi, Waziri Kairuki ameielekeza Idara ya utawala kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao ikiwa ni pamoja na maslahi na madai yao na pia kuwaelimisha kuhusu nyaraka za kiutumishi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news