Taarifa muhimu na ya haraka kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) leo

AWAMU YA PILI YA WITO KWA AJILI YA UDAHILI WA UFADHILI WA PROGRAMU YA MSINGI YA SAYANSI KWA WANAFUNZI WA KIKE

A: UTANGULIZI

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza mradi wa miaka mitano (2021/2022-2025/2026) wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation (HEET)).

Kupitia mradi wa HEET Wizara imetenga fedha kwa ajili ya ufadhili wa masomo katika Programu ya Msingi kwa wanafunzi wa kike waliopungukiwa na sifa kidogo za kujiunga na masomo ya elimu ya juu katika masomo ya Sayansi,Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STUH). Programu hiyo itatolewa katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT).

Wanafunzi watakaohitimu na kufauli masomo katika programu hii kwa viwango vilivyowekwa watapata fursa ya kuomba udahili katika taasisi za Elimu ya juu nchini kwa kufuata taratibu zilizoainishwa na TCU, NACTIVET na chuo husika, ikiwa ni pamoja na sifa za kuomba mkopo wa masomo ya elimu ya juu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania bara na Tanzania visiwani.

Waombaji wanaotoka Mikoa ambayo kijiografia haijafaidika, walemavu, yatima,familia masikini na zinazohudumiwa na TASAF na asasi zinazotambulika watapewa kipaumbele.

Maombi yaambatishe vielelezo vilivyotajwa kutoka kwa wenye mamalaka ya kutoa vielelezo hivyo kama Daktari, TASAF,RITA, serikali za mitaa pamoja na nyeti vya kuhitimu.

CKHT kinayo furaha kutangaza awamu ya pili ya nafasi za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kike wenye sifa zinazohitajika ili kujiunga na programu hii maalumu.

B: SIFA ZA KUJIUNGA

Muombaji ataweza kukubaliwa kujiunga kwenye programu husika endapo atakuwa na vigezo vingine muhimu vifuatavyo:

i. Cheti cha Mtihani wa Elimu ya Sekondari (Kidato cha NNE) kikiwa na ufaulu angalau kwenye masomo manne ambayo yamepatikana kabla ya kufanya mtihani wa juu wa Elimu ya sekondari au ufaulu unaofanania na chochote kati ya vifuatavyo:

ii. Cheti cha Juu cha Mtihani wa Elimu ya Sekondari (Kidato cha SITA) kwenye masomo ya sayansi(Fizikia, Kemia,Baolojia, Hisabati,Uchumi na Jiografia) na angalau alama 1.5 kutoka kwenye masomo MAWILI
AU

iii. Diploma katika masomo ya STUH kutoka kwenye chuo kinachotambulika yenye ufaulu wa GPA ya 2.0 mpaka 2.9.
AU

iv. NTA Level 5/Professional Technician Level II Certificate.

C: NJIA ZA KUFUNDISHA
Programu hii itafundishwa kwa njia ya ana kwa ana, mihadhara ya mtandaoni (Blended mode) na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

D: MAENEO YA UFADHILI

Ufadhili utazingatia maeneo yafuatayo: ada ya masomo, gharama za chakula na malazi, vifaa vya kujifunzia, shajara, bima ya afya, Kishikwambi, nauli ya kutoka nyumbani na kwenda kituo cha mafunzo na kurudi nyumbani baada ya kuhitimu.

E: UTARATIBU WA KUTUMA MAOMBI

Muombaji anapaswa kujaza fomu ya maombi ambayo inapatikana kwenye vituo vyote vya mikoa vya CKHT bara na visiwani (Unguja na Pemba).

Fomu ya maombi inapatikana pia kwenye tovuti ya CKHT. Fomu ikishajazwa irudishwe kwenye kituo cha mkoa husika.

Mwombaji pia anaweza kutuma fomu yake ya maombi baada ya kuijaza kupitia barua pepe ya (ofpheet@out.ac.tz) Hakuna ada ya udahili.

F: MWISHO WA MAOMBI: NOVEMBA 30, 2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news