Rais Dkt.Nabiijoshua: Mitume na manabii wote Tanzania tuna jambo kubwa Morogoro

MOROGORO-Baraza la Mitume na Manabii Tanzania (BACCT) linatarajia kufanya mkutano mkuu wa baraza hilo kuanzia Novemba 15 hadi 17, 2023 mkoani Morogoro.

Hayo yamesemwa na Rais wa baraza hilo,Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala wakati akizungumzia kuhusu maandalizi ya mkutano huo ambao unatarajiwa kuwa wa kihistoria kwa mitume na manabii nchini.

"Tarehe 15 hadi 17 Novemba, 2023 baraza letu litaandika historia mpya ya injili ya kitume na kinabii nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.

"Tunamshukuru Mungu kuwa, Serikali yetu ya Tanzania inaunga mkono kila jambo jema linalofanywa na viongozi wa dini nchini hususani wanaoombea amani ya nchi kama sisi,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.

Rais huyo wa BACCT ameendelea kufafanua kuwa, "Kama tulivyopanga kuwa kama tungefanya mkutano huu Dodoma siku ya mwisho ungefuatiwa na mkutano mkubwa wa hadhara ili kuliombea na kulibariki Taifa letu na viongozi wake.

"Ndivyo tutakavyofanya hapa Morogoro pia, tofauti ya Morogoro na Dodoma ni kwamba hapa Morogoro tumemwalika ndugu yetu Mchungaji Ezekiel kutoka nchini Kenya.

"Kwa moyo wa upendo aliojaliwa na Mungu amekubali kutoa mamilioni ya fedha ili kugharamia mkutano huo mkubwa unaotarajiwa kukusanya watu wasiopungua laki moja.

"Ni kwa ajili ya kuliombea Taifa na viongozi wake hususani mkuu wetu wa nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ili Mungu amlinde na kumpa ushindi katika mambo yote kwa masilahi mapana ya nchi yetu."

Rais Dkt.Nabiijoshua amesema, ili kufanikisha mkutano huo mkubwa kuanzia Novemba 17 hadi 19, 2023 amemteua Nabii Clear Malisa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ambapo Mchungaji Ezekiel kutoka Kenya atahubiri kwa siku tatu.

"Mkutano huo utakuwa mwanzo wa mikutano mingi isiyo na ukomo hadi kila kitu kiweze kutii amri ya Mungu wetu na kulifanya kanisa la kitume na kinabii kuwa kinara wa injili Afrika nzima.

"Tumeshakamilisha mazungumzo na wahubiri wakubwa, vijana wenzetu wa Afrika akiwemo Apostel John Chi, mtoto wa hayati TB Joshua.

"Kwamba mwishoni au mwanzoni mwa mwaka huu tuwe na mkutano mkubwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kulibariki bara letu la Afrika na watu wake.

"Mkutano huo watahudhuria maraishi wa nchi kadhaa za Afrika na mama yetu Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa mwenyeji wao, hapo ndipo wengi wataelewa maana ya msemo wa Nani kama Mama,"amefafanua Dkt.Nabiijoshua.

Rais Dkt.Nabiijoshua amesema,kuhusu mkutano huo, mtumishi wa Mungu, Nabii Lolinga atalielezea vizuri katika mkutano huo mkuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news