Waziri Simbachawene atoa maagizo TAKUKURU

RAINER BUDODI NA VERONICA MWAFISI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutafakari kwa kina na kujadili changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi na kuzifanya kuwa fursa kwa maendeleo ya Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 wa Viongozi wa TAKUKURU. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene tuzo ya kuthamini mchango wake katika mapambano dhidi ya rushwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 wa Viongozi wa Taasisi hiyo uliofanyika jijini Dodoma.

Mhe. Simbachawene amesema hayo Novemba 20, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU-2023 katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma.
“Ninaamini mtatumia fursa ya mkutano huu wa mwaka kujadili masuala yote yanayoonekana kuwa ni changamoto katika utendaji kazi ili kupata suluhu ya pamoja,” ameongeza Mhe. Simbachawene.
Sehemu ya Viongozi wa TAKUKURU na Wawezeshaji wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 jijini Dodoma.

Aidha, katika hotuba yake amebainisha kuwa kila mmoja katika mazingira tofauti na kwa namna ya pekee ameruhusu au ameathiriwa na rushwa, hivyo ametoa rai kwa wananchi wote kuhakikisha wanazuia mianya ya rushwa ili kutoathiri vizazi vijavyo.

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa TAKUKURU inatakiwa kuitumia vizuri programu iliyoianzisha ya TAKUKURU Rafiki kwa lengo la kupanua wigo na kuwashirikisha wananchi katika kupambana na rushwa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema ofisi yake inaendelea na utekelezaji wa shughuli zake kwa mujibu wa Sheria na sasa wamejikita zaidi katika kuzuia rushwa.

“Tunaendelea na kazi ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya rushwa na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo tumeokoa fedha nyingi ambazo kama isingekuwa TAKUKURU basi fedha hizo zingeishia mikononi mwa watu binafsi,” amesema Bw. Hamduni.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubainisha changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao na kutafuta ufumbuzi wa pamoja. Mkutano huu wa Mwaka kwa mwaka 2023 una kaulimbiu ya Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news