MAAFA KATESH:Hakuna haki ya muathirika itakayopotea

MANYARA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kuwahifadhi waathirika wa maporomoko ya mawe na matope kutoka Mlima Hanang’ mkoani Manyara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waathirika wa maafa ya maporomoko ya Mawe na Matope alipoenda kuwafariji na kuwapa pole.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao na viongozi wa Serikali, Wazee na Waathirika wa Maporomoko hayo katika Kijiji cha Gendabi Halmashauri ya wilaya ya Hanang’ mkoani humo.

Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha kuwa, Serikali itaendelea kutoa huduma zote muhimu kwa kila aliyeathirika na maafa hayo na kipaumbele ni wale waliohifadhiwa katika Kambi za muda zilizopo na endapo kuna mazingira rafiki ya kuhifadhiwa na ndugu, jamaa na marafiki wanapaswa kufuata utaratibu zilizopo.

“Tunahitaji kupunguza mikusanyiko mikubwa kwenye makambi kiafya siyo sahihi tutahakikisha tunamhudumia kila Muathirika popote atakapokuwa amehifadhiwa na ndugu au Jamaa na hakuna haki yake itakayopotea,” alibainisha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Viongozi wa Serikali na Waathirika wa maafa katika kijiji cha Gendabi Halmashauri ya Hanang' mkoani Manyara alipowatembelea na kuona hali inavyoendelea katika eneo hilo.

Aidha,alishauri kuwa, wananchi wawapokee waathirika wa maporomoko ya mawe katika makazi yao na hata kama nyumba itakuwa haitoshi serikali itawezesha kujenga mahema ili waweze kujitosheleza.

Alifafanua zaidi kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha vifaa vya msaada wa kibinadamu vinawafikia waathirika katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ikiwemo chakula, magodoro pamoja na mablanketi.

“Sio kweli kwamba muathirika wa maporomoko ya mawe na matope akienda kwa ndugu zile stahiki zake atakosa, cha msingi ni kuainisha eneo analokwenda kwa anuani, majina viongozi wake pamoja na mawasiliano yao,”alifafanua.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akimfariji Muathrika wa Maporomoko ya Mawe na Matope Kutoka Mlima Hanang katika Kambi ya Katesh.

Kwa upande wake Nyerere Izrael mwenyeji wa Kijiji cha Gendabi ameomba serikali kutuma wataalamu kuangalia tabia za Mlima Hanang’ ili janga hilo lisije likajirudia.

“Wataalamu watasaidia kutupa taarifa za awali kama eneo ni salama au si salama kuendelea kuishi bila kuleta taharuki kwa wananchi,"alisema.

Awali Bwana Steven Sulle Mwenyekiti wa CCM Kata Gendabi, amemshaukuru, Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, ni Rais wa kipekee kabisa na ameonesha upendo na kutoa faraja katika madhila haya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Jenista Mhagama akimfariji kijana alinusurika katika Maporomoko ya Mawe na Matope Kutoka Mlima Hanang katika kambi ya Katesh.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).

“Niipongeze Serikali kwa kutukimbilia sisi tunawashukuru sana, ila nashauri wale waathirika wenye uwezo wa kwenda kwa ndugu, jamaa na marafiki watumie utaratibu uliopo na ni sahihi kuwapokea kwa upendo, tunavyoendelea kuwaacha katika eneo la Kambi, wataendelea kuwa wapweke zaidi,” alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news