Tusipofanya maombi, 2024 wengi watalia nchini-Mwinjilisti Temba

KILIMANJARO-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amesema, mwaka 2024 si rahisi kwa Watanzania kama wanavyofikiria, kwani kupitia maombi ameoneshwa utakuwa na ajali nyingi zikiwemo imani za kishirikina.
Amesema, ili kuishinda hali hiyo,ni Watanzania bila kujali imani zao kumuomba Mungu kwa bidi ili aweze kuliepusha Taifa na changamoto hizo ambazo zinaweza kuleta maumivu makubwa.

Utabiri huo ameutoa Desemba 31, 2023 akiwa katika Viwanja vya Ushirika vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mkesha wa mwaka mpya.

“Mwaka 2024 nina unabii wa Kitaifa, si wa kifamilia, hautakuwa mrahisi kama vile wengi wanavyofikiria, hautakuwa mrahisi mwaka 2024.

“Mwaka 2024 nimeoneshwa na Bwana kwamba utakwenda kuwa na ajali nyingi za magari. Mwaka 2024 kutakuwa na ajali nyingi sana kupitia magari makubwa kwa madogo, malori ambazo zitatoa uhai wa watu wengi sana, watapoteza maisha,

“Lakini, pamoja na hayo yote yatakayotokea inatuhitaji watu tusimame ili kuvunja hii roho, lakini pia na Serikali iweze kuongeza miundombinu na njia mbalimbali nchini.

“Nataka niwaambie watanzania kwamba, nimeoneshwa wazi wazi, nimeona ajali nyingi, lakini pia ijulikane kuwa, 2024 ni mwaka wa kwenda kwenye uchaguzi.

“Nimeonyeshwa pia, matambiko yatakuwa mengi, makafara yatakuwa mengi ya damu ya watu na ya nyoka, na hii inapelekea hasira ya Mungu iendelee kuwa kubwa.

“Kwa sababu watu wanajipanga sasa hivi kuingia kwenye uongozi wapate kwa njia ya makafara, na ndiyo maana zitatokea nabii nyingi nje ya nchi ya Tanzania,zikithibitisha haya.
“Unajua wengi wetu tunadharau, Mungu hutuma watu wengine kutoka nje ya Tanzania, wataonyeshwa kuliko Watanzania juu ya haya mauaji, mauti, majanga makubwa na kadhalika ambavyo yanakwenda kutokea.

“Si jambo rahisi kama unavyofikiria, lakini pia ninataka niishauri Serikali. Lazima Serikali ikae na watu ambao Mungu amewapa karama na vipawa vya hali ya juu ili waweze kuwaambia nini ambacho kitatokea.

“Kwa sababu msipofanya hivyo, ndiyo maana Taifa linaingia kwenye matatizo kama sasa hivi, Bibilia inasema siku ya mwisho maarifa kuhusu Mungu yataongezeka, kwa hiyo kama ninyi hamtatumia nafasi hiyo kujifunza kulingana na maarifa yatokayo kwa Mungu, watu wataendelea kuangamia kwa sababu mmekosa hayo maarifa ya Mungu.

“Maarifa ya Mungu ni kitu cha muhimu sana, angalia Marekani kwenye fedha yao wanasema wanamwamini Mungu, si Tanzania tunasema tunampenda Mungu, lakini hatupo kwenye ule uhalisia wa kumkubali Mungu na kumtumikia.

"Taifa la Tanzania mwaka 2024 halitakuwa rahisi kama vile mnavyofikiria kutakuwa na mambo mengi ya ajabu ajabu, na masuala ya kiuchawi yataendelea kutawala katika siasa huku hasira ya Mungu ikiendelea kuwaka zaidi Tanzania.

“Hivyo, ninawasihi Watanzania kila mtu na dini yake aendelee kumlilia Mungu na kuachana na huu ujinga, na tuachane na haya mambo ambayo hayampendezi Mungu,”amefafanua Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news