Uvuvi haramu hapana-Rais Dkt.Samia

MWANZA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri kudhibiti na kutokomeza vitendo vya uvuvi haramu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega kuhusu aina ya samaki wanaopatikana Ziwa Victoria, hii ni baada ya kuzindua ugawaji wa boti za uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kwenye hafla iliyofanyika jijini Mwanza.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi katika uwanja wa Nyamagana mara baada ya kuzindua na kukabidhi boti za uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa.

Aidha, ameitaka Wizara hiyo kuwachukulia hatua kali za kisheria wavuvi wanaokiuka taratibu za uvuvi salama.

Pia, alisema Serikali inafanya jitihada kuinua sekta ya uvuvi nchini kwa kuimarisha utendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili iendane na dhamira ya mageuzi yaliyokusudiwa.

Vile vile, Rais Samia alisema kundi la vijana na wanawake linaongoza kushiriki kwenye ajira zisizo rasmi hivyo serikali inarasimisha shughuli zao kwa kuwawezesha kupata zana na nyenzo za kisasa ili kujikimu kiuchumi.

Rais Samia alisema, Serikali imejipanga kukuza sekta ya uvuvi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ununuzi wa meli za kisasa za uvuvi katika bahari kuu, ujenzi wa bandari za uvuvi katika maeneo ya Kilwa Masoko mkoani Lindi na Bagamoyo ili kuongeza Pato la Taifa.

Boti 160 za uvuvi wa kisasa zimezinduliwa kwa wanufaika 989 pamoja na vizimba 222 vinavyotarajiwa kugaiwa kwa wanufaika 1,213 katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news