Mafunzo ya ujuzi yagusa kaya maskini 600 Zanzibar

ZANZIBAR-Mnamo Desemba 14, 2022, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilizidua rasmi Mpango wa Ufadhili wa Mafunzo ya Ujuzi kwa Vijana wanaotoka Kaya Maskini na Wanaoishi katika Mazingira Magumu kwa upande wa Zanzibar.
Baadhi ya wanufaika wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi, Dkt. Mwanakhamis Ameir mara baada ya kutunukiwa vyeti vyao.

Mafunzo hayo yalikuwa ya muda mfupi kati ya wiki mbili hadi miezi mitatu na yalilenga kuwanufaisha vijana wanaotoka katika kaya maskini waliosajiliwa katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Mgeni rasmi Dkt. Mwanakhamis Ameir akitoa cheti kwa mmoja wa wanufaika wa Mpango wa Ufadhili kutoka Kaya Maskini waliosoma mafunzo ya amali kupitia ufadhili wa TEA. Kulia kwake ni Bw. Ephrahim Simbeye, mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Masozi Nyirenda, Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka TEA. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar. Dkt. Bakari Silima.

Mpango huo umetekelezwa kwa mafanikio makubwa sana ambapo jumla ya vijana 600 wamefanikiwa kupata mafunzo ya ujuzi katika fani mbalimali kama vile mapishi, ushoni, ufundi magari, ufundi umeme, kilimo cha mbogamboga, uchomeleaji wa vyuma pamoja na ufundi bomba.

Kati ya wanufaika hao 600, jumla ya wanufaika 300 wametoka katika kisiwa cha Unguja na 300 wametoka Pemba.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Dkt. Mwanakhamis Ameir ambaye alikuwa mgeni rasmi akitoa nasaha zake kwa wahitimu wa Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka Kaya Maskini na wanaoishi katika mazingira magumu waliofadhiliwa na Mamlaka ya Elinu Tanzania. Hafla hiyo ya mahafali imefanyika Januari 31,2024 Mkokotoni, Unguja.

Akizungumza Januari 31,2024 Kaskazini Unguja katika hafla ya kuwapongeza na kuwatunukia vyeti wanufaika hao Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Dkt. Mwanakhamis Ameir amesema, ni wakati muafaka sasa kwa wanufaika hao kwenda mtaani kuzitafuta fursa kwani tayari wana ujuzi na vyeti wanavyo.

‘‘Ni wakati wa kwenda kujichangaya mtaani sasa ili fursa ziwaone maana fursa zipo kila mahali ila sharti ni lazima utoke hapo ulipo, ufanye kitu hata kama kitakuwa hakikulipi kwa wakati huo ili ujuzi ulio nao uonekane na mwisho fursa zitakufuata," amesema Dkt. Mwanakhamis.
Sehemu ya wanufaika wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa mahafali ya vijana kutoka kaya maskini yaliyofanyika Unguja Zanzibar.

Aidha ameongeza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinatambua uwepo wa kaya masikini katika jamii zetu na zinatambua uwepo wa changamoto nyingi ambazo zinakabili familia hizo ikiwemo kipato cha chini kinachopelekea kiwango duni cha upatikanaji wa huduma za msingi.

Amesema, katika kukabilia na changamoto hiyo, Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa Kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mradi wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) iliona njia mbadala ya kupunguza au kuondoa ugumu wa maisha kwa familia za kaya maskini ni kuwapatia vijana wanaotoka katika familia hizo taaluma ya ufundi kupitia fani tofauti ili vijana hao waweze kujiajiri au kuajiriwa na kupata kipato kitakachosaidia familia zao.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bw. Ephrahim Simbeye akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka TEA,Bw. Masozi wakati wa mahafali ya vijana kutoka kaya maskini yaliyofanyika Unguja Zanzibar.

‘‘Nafarijika sana kuwa hapa leo ili kuwapongeza na kuwatunukia vyeti vijana 600 ambao wamenufaika na mafunzo ya ujuzi kupitia Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka kaya maskini. Mradi huu unaendana kabisa na vipaombele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vya kuandaa mageuzi katika sekta ya elimu kwa kuwekeza katika mafunzo ya amali,"amesema Dkt. Mwanakhamis.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi Mkurugenzi Mtendaji, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Silima amesema, kwanza anaishukuru sana TEA kwa kuwakumbuka vijana kutoka kaya maskini na kuwapa ufadhili wa huo wa mafunzo ya ujuzi.
Mkurugenzi Mtendaji, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar,Dkt. Bakari Silima akitoa taarifa jinsi mafunzo yalivyotekelezwa kwa vijana kutoka kaya maskini waliosoma mafunzo ya amali kupitia ufadhili wa TEA.

Amesema, kutokana na kipato duni walicho nacho vijana hao wengi wanakwama kuzifikia fursa hivyo wamekuwa wakiwahimiza kujiunga katika vikundi ili waweze kupata msaada kutoka kwa wadau, mashirika, taasisi na pia Serikali kupitia idara ya vyama vyama ushirika.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bw. Ephrahim Simbeye akitoa salamu kutoka kwa viongozi wa wizara katika mahafali ya vijana kutoka kaya maskini waliosoma mafunzo ya amali kupitia ufadhili wa TEA.

Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Bw.Ephrahim Simbeye amesema, mwaka 2020/2021, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia zilikubaliana kuanzisha Mpango wa Ufadhili wa Mafunzo ya Ujuzi kwa Vijana wanaotoka Kaya Maskini na Wanaoishi katika Mazingira Magumu (Bursary Scheme for Vulnerable Groups) uliowekwa kuwa sehemu ya ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) chini ya usimamizi wa TEA.

Ameongeza kuwa, katika kukabiliana na changamoto ya nguvu kazi isiyo na ujuzi wa kutosha unaotakiwa katika soko la ajira, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zimeweka mikakati mbalimbali inayolenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanakhamis Ameir ambaye alikuwa mgeni rasmi akiteta jambo na Bw. Ephrahim Simbeye mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa mahafali ya vijana kutoka kaya maskini yaliyofanyika Unguja Zanzibar.

Amesema, mikakati hiyo inalenga kufikia lengo la nane la Umoja wa mataifa la Maendeleo Endelevu linaloazimia mataifa kuchangia ukuaji wa uchumi endelevu, ajira kamili zenye tija, na kazi zenye staha kwa wote, na kuwawezesha wananchi kupata Ujuzi na fursa za kiuchumi ili kupunguza umaskini wa kipato na kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi.
Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka,TEA Bw. Masozi Nyirenda akielezea kuhusu Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka Kaya Maskini na wanaoishi katika mazingira magumu katika mahafali ya vijana hao yaliyofanyika Unguja Zanzibar.

Kwa upande wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi, Bw. Masozi Nyirenda amesema, lengo la Mpango lilikuwa kufadhili Mafunzo kwa Jumla ya Wanufaika 4,000 nchi nzima, ambapo hadi sasa jumla ya vijana 4,063 wameshanufaika, ikiwemo vijana 600 wa Zanzibar ambao wamekabidhiwa vyeti vyao.

Mpango wa Ufadhili wa Mafunzo ya Ujuzi kwa Vijana kutoka Makundi Maalumu na Wanaoishi katika Mazingira Magumu ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund -SDF) chini ya Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi kwa ajili ya Ajira zenye Tija (Education and Skills for Productive Jobs-ESPJ) unaoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mgeni rasmi Dkt. Mwanakhamis Ameir akitoa cheti kwa mmoja wa wanufaika wa Mpango wa Ufadhili kutoka kaya maskini waliosoma mafunzo ya amali kupitia ufadhili wa TEA.

Mfuko wa SDF ulikuwa unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news