Msajili wa Hazina Zanzibar asisitiza ufanisi kwa taasisi, mashirika

ZANZIBAR-Msajili wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waheed Ibrahim Muhammed Sanya amewataka watendaji wa taasisi mbalimbali na mashirika ya umma kushirikiana na ofisi hiyo ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.
Sanya ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa kuwajengea uelewa watendaji wakuu wa taasisi za uwekezaji wa umma katika Ukumbi wa Zura Maisara jijini Zanzibar.

Amesema, kikao hicho kitawawezesha kufahamu majukumu yao pamoja na kujua Ofisi ya Msajili wa Hazina ina nafasi gani katika utendaji wao.

Amesema, taasisi hiyo ni kubwa inayofanya kazi kwa karibu na taasisi nyingi za Serikali hasa zinazozalisha, hivyo ni wajibu wao kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo nchini.

Amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kujenga uelewa kwa watendaji wa taasisi hizo juu ya kazi zinazofanya na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na kuwapatia fursa ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika taasisi zao na kuzipatia ufumbuzi.

Pia,  amesema ofisi hiyo ina mpango wa kuwapatia mafunzo ya muongozo kwa baadhi ya watendaji ili kuwajengea uwezo na kuleta mabadiliko chanya katika taasisi zao.

“Endapo watendaji wakuu wa taasisi hizi watakua na uelewa mzuri juu ya ofisi hii wataweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwa mabalozi wazuri kwa wanaowaongoza,”amesema Sanya.

Akiwasilisha mada ya mahusiano baina ya ofisi na mashirika ya umma na mpango kazi wa ofisi hiyo, Kaimu Mkuu wa Mashirika ya Uwekezaji ya Umma, CPA Mussa Ali Juma amesema kuwa, Serikali inatoa gawio kwa taasisi zake kupitia uchangiaji wa taasisi hizo ili kuendeleza utendaji kazi wao na kuleta maslahi kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Akitoa ufafanuzi kuhusu Ofisi ya Msajili wa Hazina, CPA Mussa amesema kuwa,  kuna haja ya kufanya muongozo mmoja katika taasisi kutokana na uwepo wa miundo tofauti katika taasisi hizo.

Amesema, lengo ni kuona taasisi hizo zinafanya uwekezaji mzuri kwa maslahi ya Taifa, kwani ndio wenye jukumu la kutoa muongozo na kusimamia mali za umma katika taasisi hizo.

Ameongeza kuwa, kazi yake kubwa ni kuruhusu kutumia au kuondolewa kwa mali za umma pamoja na kutoa muongozo utakaoelekeza namna nzuri ya kuongoza taasisi zao.

Nao washiriki wa mkutano huo wameahidi kutoa ushirikiano wao katika ofisi hiyo sambamba na kukubaliana katika utendaji wa kazi zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news