Prof.Mwegoha aongoza mamia waombolezaji kumuaga Mhadhiri wa Mzumbe,Balozi Dkt.Kamala

DAR ES SALAAM-Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Februari 17, 2024 katika Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko - Dar es Salaam ameungana na ndugu, jamaa na marafiki, katika kuuaga mwili wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala aliyefariki dunia tarehe 12 Febuari 2024.
Prof. Mwegoha amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahya – Othman, ambao kwa pamoja wamemwelezea Marehemu Balozi Kamala kama kiongozi aliyekuwa na maono ya kimkakati katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa ndani na nje ya nchi, kujenga amani na kuleta maendeleo kwa Tanzania kupitia nyadhifa mbalimbali alizoshika enzi za uhai wake.
“Tukio hili si jepesi kulipokea hasa ukizingatia mahusiano mema ambayo marehemu aliyejenga na wafanyakazi wenzake, wanafunzi na watu mbalimbali waliobahatika kukutana naye. Pia, ni pigo kubwa kwa jamii yetu na kwa nchi ya Tanzania kwa ujumla kupoteza kiongozi mwenye uzoefu na mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali hususan kwetu sisi wanataaluma,”amesisitiza Prof. Mwegoha.
Amesema, Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala atakumbukwa sana kwa mchango mkubwa kwa Chuo Kikuu Mzumbe toka alipokuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (IDM-Mzumbe), akiwa mtu aliyeipenda sana kazi yake katika kuongoza kundi kubwa la wanachuo na kuajiriwa kama Mkufunzi mwenye ufahamu wa hali juu katika masuala ya uchumi.
“Mchango wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala bado unaishi na utaendelea kuishi kupitia kazi nyingi za kitaaluma na kisiasa alizozifanya. Moja ya vitu vinavyofariji ni sifa aliyokuwa nayo ya kupenda kuyaweka mawazo yake katika maandishi. Hii inatusaidia kubaki na rejea ya mambo aliyoyafahamu, vitu alivyoviamini na mawazo aliyoyajenga juu ya mambo mbalimbali,”amesisitiza Prof. Mwegoha.
Awali, Paroko wa Kanisa la Mwenyeheri Isidori Bakanja Padri Emmanuel Makusalo na Padri Florence Rutaihwa Rwehumbiza kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania walioendesha ibada ya misa ya mazishi, kwa pamoja, wamewataka waamini na waombolezaji kujiandaa na kifo kwa kudumu katika sala ili waweze kukikabili vema kwa kuwa hakuna ajuaye siku wala saa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news