Shule za kata ni zake

NA LWAGA MWAMBANDE

FEBRUARI 13, 2024 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango aliwaongoza viongozi na wananchi katika kutoa heshima za mwisho kwa Waziri Mkuu Mstaafu hayati Edward Ngoyai Lowassa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt.Mpango alitoa pole kwa familia, ndugu, marafiki pamoja na watanzania wote kwa ujumla kufuatia msiba huo mkubwa kwa Taifa.

Pia, Makamu wa Rais Dkt.Mpango alisema, Serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa aliyoutoa hayati Edward Lowassa katika maendeleo ya nchi kwa kuwa alijitolea kwa dhati kulitumikia Taifa pamoja na kutumia vema karama alizojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika.

Alisema, ni muhimu kila mtanzania kujikumbusha wajibu aliyonao kwa taifa na kuyaishi kwa vitendo mambo yote mazuri yanayotokana na maisha ya hayati Lowassa.

Vile vile, Makamu wa Rais alisema ni vema Watanzania kumuenzi hayati Lowassa kwa kuendelea kuchapa kazi ili kuboresha maisha na hivyo kuchangia katika ujenzi wa Taifa kwa kuwa alikuwa mchapa kazi hodari katika utumishi wa umma na katika shughuli zake binafsi ikiwemo ufugaji.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa watanzania wote na hususani vijana kumuenzi hayati Lowassa kwa kutumia fursa mbalimbali kujipatia elimu kwa manufaa ya Taifa kwa kuwa alikua kinara katika elimu na kusimamia kwa uhodari utekelezaji wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ya elimu hususani ujenzi wa shule za sekondari kila kata.
   
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, hayati Edward Ngoyai Lowassa ameondoka akiwa ameacha alama kubwa kwa Taifa, kwani alifanya kazi yake, sisi tunakula matunda kwa sasa. Endelea;

1.Aondoka enda zake, zinabaki sifa zake,
Wanaume wanawake, wengi wanasema yake,
Hiyo ni alama yake, yabaki aenda zake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

2.Hiki umuhimu wake, acha niliseme peke,
Kwa Lowassa kazi yake, katika uhai wake,
Hili vema tutamke, kaacha alama yake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

3.Shule za kata ni zake, wazo lake kazi yake,
Tufurahie tucheke, watoto waelimike,
Ni vema ifahamike, Lowassa kaenda zake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

4.Hali ilikuwa mbaya, Kikwete wakati wake,
Shule chache angaliya, watoto watawanyike,
Wawili hawakugwaya, sekondari wasimike,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

5.Uamuzi kila kata, iijenge shule yake,
Ni sekondari za kata, nchini tuzisimike,
Lowassa lipitapita, mtu asikengeuke,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

6.Kwa sasa watoto wengi, hatutaki wachepuke,
Shule zimekuwa nyingi, lazima waelimike,
Tena na ajira nyingi, walimu waajirike,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

7.Sasa wahitimu wengi, kutokea shule zake,
Wapo waupiga mwingi, kiuchumi tuibuke,
Ni kwa ule umuhimu, zile jitihada zake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

8.Mesoma shule ya kata, na Lowassa mkumbuke,
Jinsi alivyochakata, kwamba shule zijengeke,
Sasa ukipitapita, nyingi hata usitake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

9.Kitu akisimamia, ni lazima kifanyike,
Kama hujamjulia, utajua usitake,
Sasa ametangulia, mwache akapumzike,
Alifanya kazi yake,sisi twayala matunda.

10.Unazikwa mwili wake, na kuonekana kwake,
Walakini kazi zake, katika maisha yake,
Ni zetu siyo za kwake, zinabaki zitumike,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

11.Sasa yamekwisha yake, na ya kwetu tuyaweke,
Kesho tuje tutajike, majina tuyasimike,
Wajao wafaidike, nasi tukaongeleke,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news