TAWA yazidisha heshima kwa wananchi Kilwa, utalii unaipa Serikali fedha nao wanafaidi

NA BEATUS MAGANJA

MKUU wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Mhe. Christopher Emil Ngubiagal amesema,Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ni taasisi iliyoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Utalii na kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali

Sambamba na wazawa wa wilaya hiyo kutokana na maboresho ya miundombinu ya utalii katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara yanayopelekea watalii wengi kutembelea Hifadhi hiyo.
Komredi Ngubiagal ameyasema hayo Februari 25, 2024 akizungumza na waandishi wa habari wilayani humo ikiwa ni siku moja baada ya meli iliyobeba watalii 146 kutia nanga katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara.
"Naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa awamu ya sita kwa kuona sasa utalii katika wilaya ya Kilwa ni vyema tupeleke taasisi inayoitwa TAWA ili kusudi ikasimamie, ikaendeleze, ikaboreshe hii Sekta nzima ya utalii ya wilaya ya Kilwa," amesema Mhe. Christopher Ngubiagal.
"Kwa kweli kwa sasa hivi unavyoona maendeleo makubwa katika Sekta hii ya utalii Kilwa yameletwa na Taasisi ya TAWA, Leo ukifika Kilwa kisiwani utaona mabadiliko makubwa katika miundombinu," ameongeza Mkuu huyo wa wilaya.

Mhe. Christopher amesema, awali kabla ya ujio wa TAWA wakazi wa wilaya yake pamoja na watalii walikuwa wakipata adha ya kufika Kilwa kisiwani kutokana na uduni wa miundombinu lakini baada ya kuingia TAWA walipeleka boti za Kisasa ambazo zinawafanya watalii na wazawa hao kufika hifadhini kwa raha mstarehe.
Aidha,amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza soko la utalii aliposhiriki filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea.
Naye Said Amri Said mkazi wa Kilwa kisiwani amekiri kuwa ujio wa TAWA katika Hifadhi hiyo umechangia kuongeza idadi ya watalii ambapo kupitia wageni hao wakazi wa eneo hilo wananufaika kiuchumi kwa kufanya biashara ndogo ndogo ambazo zinawaingizia kipato.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja ametoa wito kwa wakazi wa wilaya ya hiyo kutumia fursa ya ujio wa Meli za watalii kujiongezea kipato kwa kuuza bidhaa pendwa kwa wageni kama vile vitu mbalimbali vya asili na kiutamaduni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news