Kuna ongezeko la wawekezaji maeneo ambayo hayakuwa na mvuto-TANAPA

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Juma Kuji amesema, katika hifadhi za Taifa kumekuwepo na ongezeko la wawekezaji kwenye maeneo ambayo yalikuwa hayana mvuto kwa wawekezaji zikiwemo Hifadhi za Ruaha, Saadani na Mikumi.

Amesema, jumla ya maeneo mapya ya uwekezaji 176 (34 ni loji na 142 ni kambi) yameainishwa katika hifadhi zote kwa kuzingatia mipango ya uendeshaji wa kila hifadhi na yametangazwa kwenye tovuti ya shirika.
Ameyasema hayo leo Machi 21,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi cha wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Nitoe pongezi kwa Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi mahiri na juhudi kubwa anazozifanya katika kuimarisha na kukuza sekta ya uhifadhi na utalii nchini katika kipindi chake cha uongozi wa nchi kwa miaka hii mitatu.

"Pia, nitumie nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuliwezesha shirika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa."

Vile vile, Kamishna Kuji amesema,kumekuwepo na ongezeko la bidhaa za utalii katika maeneo mengine ambayo awali hayakuwa na bidhaa husika.

Miongoni mwa bidhaa hizo ni kuongezeka kwa wigo wa shughuli za utalii wa puto kutoka kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda hifadhi za Tarangire, Ruaha na sasa maandalizi yanaendelea kwa Hifadhi ya Mikumi;

"Utalii wa faru katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi, utalii wa baiskeli katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha.

"Nyingine ni utalii wa michezo na burudani katika Hifadhi ya Taifa Serengeti mchezo wa tennis na Hifadhi ya Taifa Mikumi mpira wa miguu, pete na kikapu."

Amesema, pia kuna ongezeko kwa mbio za Marathon katika maeneo ya ndani na pembezoni mwa hifadhi za Taifa ambapo zimekuwa zikivutia washiriki wengi na wakati huo huo kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo husika.

"Hifadhi zilizofanikiwa kuratibu mbio za Marathoni ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Arusha, Mkomazi, Ruaha, Katavi, Mahale, Gombe, Burigi- Chato na Kilimanjaro."

Wakati huo huo, Kamishna huyo amesema,mwaka 2018 TANAPA iliingia katika mchakato wa kutambuliwa na Shirika la Viwango Duniani ili kujijengea kuaminiwa na wateja.

Amesema, kutambuliwa kwa TANAPA mwaka 2021 na Mfumo wa Utoaji wa Huduma kwa kiwango cha Kimataifa (ISO) kumewezesha wateja kuamini na kuchagua huduma zinazotolewa na shirika ikiwemo hifadhi zake hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato.

"Katika miaka mitatu, shirika limeendelea kutekeleza shughuli za utalii na uhifadhi kwa kuzingatia matakwa ya kiwango cha ubora cha ISO 9001:2015 kinachohusu utoaji wa huduma bora kwa wateja."

Kamishna huyo ameendelea kufafanua kuwa, TANAPA imeendelea kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kukamilisha ujenzi wa lango la kisasa la Naabi lenye uwezo wa kupokea zaidi ya magari 600 na wastani wa wageni zaidi ya 1,500 kwa siku.

Amesema, katika kipindi cha miaka mitatu, TANAPA pia imeweza kujenga malango mapya 10 na ya kisasa katika hifadhi za Taifa Tarangire (2), Mkomazi (3), Serengeti (2) na Nyerere (3).

"Na TANAPA imekuwa ikishinda tuzo za uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwa kufuata viwango vya kimataifa kwa upande wa taasisi za umma zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

"Shirika limekuwa mshindi wa pili wa tuzo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu za mwaka 2022 katika kundi la taasisi za kiserikali zinazotumia mfumo wa IPSASs (2nd winner in the government agencies category (users of IPSASs) for the best presented financial statements award for the year 2022)."

Ameongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya Ujerumani (KfW), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imeendelea kuboresha kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege vilivyopo katika Hifadhi za Taifa.

Kamishna Kuji amesema, shirika lina mtandao wa barabara ambao umeongezeka kutoka urefu wa kilometa 7,638 mwaka 2021 na kufikia urefu wa kilometa 16,471 mwaka 2024.

"Kazi nyingine za miundombinu zilizofanyika ni pamoja na kukarabati wastani wa kilometa 3,938 za barabara, kutengeneza njia za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 334.

"Nyingine ni ujenzi wa madaraja 14 na vivuko 399, kukarabati viwanja vya ndege (Airstrips) 11 katika maeneo ya barabara za kuruka na kutua ndege (runway) na viungio vyake pamoja na maegesho ya ndege kwa kiwango cha changarawe katika hifadhi za Serengeti (1),

"Nyerere (3), Tarangire (1), Mkomazi (2), Saadani (1), Mikumi (1) na Ruaha (2). Aidha, viwanja vya kutua helikopta (helipads) katika Mlima Kilimanjaro vilijengwa kwa kiwango cha zege kwa kuzingatia kanuni za TCAA na ICAO.

"Kununua mitambo 59 ya aina mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Benki ya Dunia (Mradi wa REGROW) na IMF (Mradi wa TCRP)."

Amesema, mitambo iliyonunuliwa kupitia mradi wa mradi wa kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii Kusini mwa Tanzania (Resilient Natural Resources Management for Tourism and Growth - REGROW) ni motor grader 5,

Pia, compactor 3, low loader 2, malori 17, excavator 2, bulldozers 2, concrete mixers 5, matrekta 7, malori ya kubebea maji 5, magari ya sinema (cinema vans) 4,

Magari ya kutolea elimu kwa wanafunzi na jamii “expedition trucks” 3 na malori ya kutengenezea magari (mobile workshop) ambapo jumla ya shilingi 27,873,761,395.00 zilitumika kununua mitambo hiyo.

Amesema, mitambo iliyonunuliwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TCRP) ni motor grader 5,

Compactor 4, low loader 4, malori 15, excavator 4, magari madogo 7 (Landcruiser), concrete mixer 1, Back low loader 1 na malori ya kubebea maji 4) vyenye thamani ya shilingi 17,765,532,026 zilitumika kununua mitambo hiyo.

"Mitambo hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu ya barabara katika hifadhi zetu,"amesema Kamishna huyo.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni taasisi ya umma ambayo ipo chini ha Wizara ya Maliasili na Utalii, lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 412 (National Parks Act Cap. 282) na marekebisho Na. 282 ya 2002 yenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa.

Maeneo ya Hifadhi za Taifa yanawakilisha kiwango cha juu kabisa cha uhifadhi wa wanyamapori nchini (highest conservation status of wildlife) ambapo hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazoruhusiwa kufanyika.

Hadi sasa Shirika linasimamia hifadhi za Taifa 21 zenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na asilimia 10.2 ya eneo lote la nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news