Muhimbili yaja na Mpango wa Dharura kuhudumia wanachama wa NHIF

DAR ES SALAAM-Kufuatia baadhi ya hospitali kusitisha huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuanzia Machi 1,2024 uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umekuja na mpango wa dharura wa kutoa huduma kwa wanachama hao ili waweze kuwa na mwendelezo wa huduma hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema hospitali imefanikiwa kuhamia kwenye kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023 kilichopendekezwa na NHIF ambapo huduma zinaendelea kutolewa.

Prof. Janabi amesema, hospitali imeongeza muda wa kuona wagonjwa katika kliniki zote za Upanga kupitia vyumba 75 vya kuona wagonjwa na vyumba vya kuona wagonjwa 59 viliyopo Mloganzila kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nne usiku au mpaka mgonjwa wa mwisho atakapomaliza kuonwa na daktari.

“Tunajua kuna wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji (electives) tunavyo vyumba 18 vya upasuaji Upanga na Mloganzila vyumba vya upasuaji 13. 

"Kwa wagonjwa wenye tatizo la figo wanaohitaji kusafishwa damu, Upanga tunazo mashine 47 za kutoa huduma hiyo na tumeongeza zamu (sessions) za kutoa huduma hiyo.

"Ni katika mzunguko wa saa nne wa kila zamu kutoka tatu hadi nne kwa Upanga na Mloganzila ambapo kuna mashine 12 tumeongezea mizunguko kutoka miwili hadi minne na muda unaobaki ni wa kufanya matengezo kinga pamoja na usafi wa mashine hizo,” ameeleza Prof. Janabi.

Prof. Janabi amesema,MNH kama mmoja wa watoa huduma wakubwa nchini nayo itaendelea kufuatilia utendaji wa kitita hicho ili kubaini changamoto zitakazojitokeza na kuziwasilisha katika mamlaka husika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news