Wazee ACT Wazalendo wapewa rai

DAR ES SALAAM-Ngome ya Wazee wa Chama cha ACT Wazalendo imetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umoja na mshikamano ndani ya chama na jamii kwa ujumla ikiwemo kuwa na sauti ya pamoja katika kutetea maslahi mapana ya Taifa.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salam na Mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Profesa Azaveri Lwaitama wakati akifungua mkutano mkuu wa pili wa Chama hicho ambao umeenda sambamba na kuchagua viongozi wa nafasi mbalimbali katika ngome hiyo.

Alisema, ni vyema wajumbe wa mkutano huo kuchagua viongozi ambao wanauwezo wa kuongoza na kuacha tabia ya kuchagua viongozi kwa mfumo kwani matokeo yake wanakosekana viongozi bora wanaoweza kuongoza katika misingi inayotakiwa kwa busara na hekima.

"Mkitaka kufika mbali lazima uwe na sauti ya pamoja hata kama mnatofautiana kwa itikadi ya vyama vyenu lakini linapokuja suala la kutetea maslahi ya nchi lazima mshikamane, hamwezi kuondoa chama kilicho madarakani kwa kujitenga,"alisema Prof. Lwaitama.

Akitoa salamu katika mkutano huo, Kamishna Msaidizi Mstaafu wa Jeshi la Polisi SACP Jamal Rwambo amesema mifumo ya vyama vya siasa nchini bado ni tatizo, hivyo kama upo katika chama cha Act Wazalendo wanachama wanatakiwa kuukataa kwa vitendo kwani unakwamisha sana kupata viongozi bora ndani ya chama.

"Mfumo wa rushwa unawaweka pembeni watu ambao wangeweza kulisaidia taifa kwa uongozi wao, wachagueni watu wenye sifa kiongozi mzuri anaeweza kuisaidia ngome ya wazee ni yule ambae ni mkweli na sio muongo," alisema SACP Rwambo.

Awali akitoa salamu za Chama cha ACT Wazalendo Mshauri wa Chama hicho, Juma Sanani amesema kuwa Wazee ndio kila kitu kwenye uongozi hivyo vijana wanapopewa ushauri wanatakiwa kuuzingatia kwani chama hicho hakina maslahi kwa mtu binafsi bali kwa wanachama wote.

Aidha, amewaomba wasimamizi wa uchaguzi huo kuhakikisha unakua wa huru na haki na kuzingatia ubora na viwango vya kimataifa, huku akiwataka wazee hapo kutumia hekima na busara katika kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaoongoza chama kwa maslahi ya Taifa.

Mapema akizungumza katika mkutano huo Sheikh Issa Ponda amesema wazee wana mambo mengi hivyo vijana wanaposhauriwa ni busara kuwasikiliza kwani hata wakiandika vitabu watu wakavisoma wataweza kujifunza vitu vingi sana.

"Wazee ndio chimbuko la fikra nzuri kwa hiyo wanatakiwa washirikishwe kwenye kila jambo, uchaguzi makini uzingatie uhalisia tunaoufahamu kuweni mfano mzuri wa kuigwa,"amesema Sheikh Ponda.

Naye, Askofu Mwamakula amesema kuwa asimilia kubwa ya wananchi wanapokuona kwenye siasa unahutubia kiongozi wa dini wanakujaji kama wewe ni mwanachama wa chama fulani kumbe uhalisia haupo hivyo inawezekana umealikwa tu, hakuna ukweli hata asilimia moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news