Tunatengeneza mikakati mbalimbali kuhakikisha Uchumi wa Kidigitali unalinufaisha Taifa na Watanzania wote-Dkt.Mwasaga

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Tehama (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema, wanaendelea kutengeneza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha Uchumi wa Kidigitali unalinufaisha Taifa na Watanzania kwa ujumla.
Dkt.Mwasaga ameyasema hayo leo Machi 26,2024 katika kipindi cha Kumekucha ambacho kimerushwa mubashara na Runinga ya ITV jijini Dar es Salaam.

Katika kipindi hicho, kiliangazia juu ya Kongamano la Tatu la Ulinzi Mtandaoni ambalo linatarajiwa kufanyika kati ya Aprili 4 hadi 5,mwaka huu jijini Arusha.Jisajili hapa》》》》

Akizungumzia kuhusu wanachoratibu kwa upande wa Tehama,Dkt.Mwasaga amesema, "Kwa mfano sasa hivi tunaangalia kuna suala linalohusiana na Mapinduzi ya Kidigitali au Digital Transformation.

"Na kwenye Digital Transformation vinaangaliwa vitu vitano kuhakikisha kwamba mambo yanaenda vizuri, cha kwanza ujuzi.

"Ujuzi wa Watanzania wote katika masuala ya kimtandao, tukisema ujuzi maana yake tunamaanisha watu wote.

"Pia, kuangalia masuala ya usalama wa kimtandao na kwamba watu wanaweza kuiamini mitandao.Hilo ni eneo lingine ambalo tunaliangalia vizuri.

"Pia,tunaangalia masuala ya kupeleka huduma za mawasiliano kwa wananchi popote pale walipo yanakwendaje.

"Cha nne, kuna Uchumi wa Kidigitali wenyewe sasa tunaujenga.

"Sasa hivi tunatengeneza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunaujenga kwa haraka sana ili Tanzania iwe shindani.

"Halafu, kitu cha mwisho tunaangalia masuala ya ubunifu kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa wabunifu hasa vijana ambao wana uwezo mkubwa sana wa mambo haya kuhakikisha kwamba tunakuwa na kampuni kubwa.

"Kwa sababu katika Uchumi wa Kidigitali wa Dunia nchi zinashindana kwa kampuni ngapi zinazotoa huduma, zinazoweza kutoka nje ya mipaka ya Tanzania na ikiwezekana hata duniani kote."
"Ukiangalia Uchumi wa Kidigitali ulivyo duniani, labda tuanzie kuanzia miaka ya 1997 wakati tunahama katika mawasiliano yalikuwa yanatumika kwa kutumia simu za mezani.

"Kama unakumbuka, na kuanza kufanya mageuzi yaliyoanza kutokea mwaka 2003 ambapo ndiyo tukaanza kuibua taasisi mbalimbali kujenga mkongo, tuliwekeza katika miundombinu kwa kiasi kikubwa sana.

"Sasa hivi ukiangalia watu katika shughuli mbalimbali wanazofanya wanatumia sana simu janja au wanatumia kompyuta au laptop kufanya shughuli zao nyingi.

Sasa kwa kuwa, hiyo sehemu imeanza kuwa na watu wengi imeshajitengeneza kama ni soko.

"Ndiyo maana unaweza kuona sasa hivi kuna huduma mbalimbali zimeweza kutengenezwa kwa kutumia mitandao kwa mfano tunapotumia usafiri.

"Kuna kampuni mbalimbali zimeweza kufanya bunifu, zingine siyo kampuni za Tanzania, tunaangalia jinsi ambavyo tunafanya malipo siku hizi tunatumia mitandao.

Kwa hiyo, hilo ni soko. Kwa kuwa hilo ni soko na kwa kuwa Afrika ukiangalia kwa kiasi kikubwa inaanza kuwa na mwingiliano wa mawasiliano, nchi zinazungumza kwa pamoja tumeshaunganishwa kwa kiasi kikubwa.

"Sasa soko linaanza kukuwa, unajua mtu yeyote unayempelekea mawasiliano akishaaza kutumia mawasiliano huyo naye anakuwa ni sehemu ya soko.

"Sasa katika haya masoko inatakiwa na sisi tuanze kutengeneza bunifu mbalimbali tuweze kupata masoko ya Kenya, Uganda, Rwanda, Congo hata ya nchi zingine za mabara mengine duniani.

"Kwa hiyo, hilo ndiyo jambo letu kubwa moja wapo ambalo tunatakiwa tulifanye na kwenye uratibu wetu ni kuhakikisha haya mambo yote yanaweza kufanikiwa kwa kufanya vitu mbalimbali,"amefafanua kwa kina Dkt.Mwasaga.

Vile vile, kongamano hilo ni sehemu ya mikakati ya Tume ya Tehama na Serikali kwa ujumla kuimarisha usalama mtandaoni ili uchumi wa Tanzania uweze kupaa na kuwa endelevu.

"Moja ndiyo kama haya makongamano tunakutana na watu mbalimbali wakiwemo Watanzania na watu wa nje kuhakikisha kwamba tunabadilishana mawazo.

"Cha msingi ni kwamba katika eneo la ulinzi tayari tuna makampuni ya Kitanzania ambayo yana soko katika bara letu la Afrika ambayo yameundwa na vijana wetu wa Kitanzania wanafanya vizuri.

"Sasa tukikutana sehemu kama hizo tunakuwa tunajadiliana, tunawaalika wanafunzi na wenyewe wanaona kwamba haya mambo yanawezekana, hili vitu vianze kwenda vizuri na kitu cha ujumla tuhakikishe tuna mtandao ambao ni salama,"ameongeza Dkt.Mwasaga.

Kongamano hilo litashirikisha zaidi ya wataalamu 300, kati yao 100 kutoka katika mataifa mbalimbali yenye kujikita katika Tehama ikiwemo Estonia.

Hivi karibuni, Dkt.Mwasaga alisema pamoja na Tanzania kuwa ni ya pili kwa usalama mtandaoni barani Afrika ikitanguliwa na Mauritius ni lazima kuendelea kuhakikisha kwamba usalama unaendelea kutokana na kuibuka kwa teknolojia mpya zinazofungamanishwa na teknolojia ya Tehama.

Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kupitia Global Cybersecurity Index limeiweka Tanzania katika nafasi ya pili Afrika baada ya kukidhi vigezo zaidi ya 150. Tanzania pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la ITU.

Kuhusu ICTC

"Tume ya Tehama ni taasisi ya Serikali na ilianza mwaka 2015, kazi zetu kubwa ziko mbili, ya kwanza ni kuratibu utekelezaji wa Sera ya Tehama ya Taifa na kazi kubwa ya pili ni kukuza Tehama

"Sisi tunawasajili wataalamu wa wote wa Tehama na kuwajengea uwezo, tunakuza kampuni ndogo ndogo chipukizi za Tehama kwa kiiingereza tunaziita Startups.

"Tunazisajili na vile vile tunazitengenezea fursa mbalimbali waweze kukua, cha tatu ni kuhakikisha kwamba Tehama inatumika vizuri katika mapinduzi mbalimbali ya kiuchumi katika mikoa yote ya Tanzania.

"Kwa sababu kwa hali halisi sasa hivi Tehama ipo sana katika miji mikubwa, na kazi kubwa nyingine ya nne ni kuifanya Tanzania kuwa shindani kwenye Uchumi wa Dunia wa Kidigitali.

"Sasa hizo ndiyo kazi zetu kwa ujumla wake, sasa kwa kufanya hivyo tunafanya nini? Tunavutia uwekezaji, hiyo ni moja kati ya kazi zetu sisi.

"Tunatengeneza programu za Kitaifa za kuhakikisha hayo yote yanaweza kufanikiwa, tunahusika na mambo ya kuhakikisha kwamba kunaku na ulinzi kwenye masuala ya kimtandao.

"Lakini kama nilivyosema katika kuratibu tunashirikiana na taasisi mbalimbali ambazo zipo zinafanya hayo mambo, kwa hiyo sisi ni wasimamizi wa Tehama nchini.

"Kazi yetu kubwa ni kuratibu sehemu mbalimbali, wizara yetu inaangalia kwa ujumla mambo yote yanaendaje katika sekta mbalimbali zinazoangukia kwenye wizara hii,"amefafanua Dkt.Mwasaga.

Ulinzi

Kuhusu ulinzi mtandaoni, Dkt.Mwasaga amesema, "Kiujumla tuna sura mbalimbali ambazo tunatakiwa tuziangalie vizuri.

"Kuna ulinzi kwanza wa kuhakikisha hiyo mifumo inakuwepo na inatoa hizo huduma kama inavyotakiwa kutolewa.

"Kwa mfano kama kampuni yenu (IPP) mmekuwa mnatoa huduma kwa muda mrefu kwa kutumia njia mbalimbali.

"Moja wapo kwa kutumia streaming kwenye mitandao na hizo huduma zipo na zinaendelea kuwepo, sasa huo upande ni watu ambao wanapeleka huduma kwa wananchi.

"Sasa, kuna wale wapokeaji wa huduma, sasa wale wanatakiwa kupewa elimu zaidi ya kuweza kujilinda na vitu gani ambayo mtu anatakiwa kuvifanya kuhakikisha wanapata huduma vizuri.

"Kwa hiyo, kuna pande mbili, kuna pande moja kuhakikisha kwamba hizi huduma zote tunazozitoa kwa kutumia mitandao zinaweza kuwepo muda wote.

"Halafu, upande wa wale walaji wa hizo huduma ni kuweza kupewa elimu vizuri ya vitu gani wanaweza kuvifanya kwenye mitandao ili waendelee kupata zile faida kubwa ambazo hizo huduma mbalimbali zinahakikisha zinafanya hivyo.

"Kama kwa mfano kwenye masuala ya malipo, elimu kwa kutumia mtandao, biashara kupitia Instagram na sehemu zingine ili kuweza kupata watu wanaweza kununua bidhaa zao na vitu vingine.

Kwa hiyo, usalama upo katika pande zote. Hili huduma iweze kumfikia mwananchi kuna mnyororo hapo upo, kwanza kwa mfano wewe uliyebuni hiyo huduma.

"Ile huduma yako inatakiwa iwe na vitu fulani, kuhakikisha kwamba yule mlaji wa huduma yako akiwa anajisajili kwenye huduma yako taarifa zake zinaweza kulindwa na vitu kama hivyo,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama,Dkt.Nkundwe Mwasaga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news