Waziri Mkuu akagua athari za maafa Rufiji

PWANI-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi waliokumbwa na adha ya mafuriko nchini waendelee kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kuratibu utoaji wa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole wananchi wa Kata ya Chumbi wilayani Rufiji, mkoani Pwani wakati alipokagua athari za mafuriko kwenye eneo hilo. Hadi sasa waathirika 740 wako kambini. Aprili 16.2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Barabara ya Mkongo hadi Utete na ile ya kutoka Mloka Mkongo zote zimeathirika. Tunafanya kazi ya kurejesha mawasiliano ili wananchi waweze kupata huduma muhimu,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa wito huo jijio ya Jumanne, Aprili 16, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Chumbi, wilayani Rufiji, mkoani Pwani ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko kwenye eneo hilo. Hadi sasa waathirika 740 wako kambini.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Ikwiriri, Rufiji akitokea Mlimba, Morogoro aliwaomba wananchi hao waendelee kutulia kwani serikali iko nao na itaendelea kuwahudumia hadi hali yao irejee katika hali ya kawaida.

“Naomba mpokee salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunatambua kuna watu wamepoteza mali na wengine mifugo,” amesema.

Amewataka watendaji wa vijiji waendelee kubaini maeneo mapya ya kuishi ambayo yatatumika kuhamisha kaya zilizoathirika. “Watendaji wa vijiji tuainishe maeneo mapya ya kwenye miinuko ili baadaye watu waweze kuhamishiwa huko,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza TARURA, TANROADS na TAZARA zishirikiane kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyopata athari wakati Serikali inasubiri kumalizika kwa mvua ili iweze kufanya ukarabati mkubwa.

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi (OWM-SBU) Bi. Ummy Nderiananga, Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi na watendaji wengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news