VIENNA-Waziri wa Nchi anayeshugulikia Mambo ya Ndani na Maendeleo wa Singapore Mhe. Dkt. Mohammad Faishal Ibrahim ameeleza dhamira ya Serikali ya Singapore kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya nchini.
Dhamira hiyo ilielezwa wakati wa mazungumzo ya uwili yaliyofanyika tarehe 11 Machi, 2025 jijini Vienna, Austria baina ya Waziri huyo na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa (Vienna), Mhe. Naimi Sweetie Hamza Aziz pembezoni mwa Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Kudhibiti Dawa za Kulevya unaondelea Jijini Vienna.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na ujumbe wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambao upo Vienna kushiriki Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Kupambana na Dawa za Kulevya.