DODOMA-Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso amewataka wataalamu wa Wizara ya Maji kuhakikisha wanaongeza nguvu ya utafiti wa kina wa maji katika Jiji la Dodoma ili kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Jiji la Dodoma.

“Ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunatatua changamoto ya maji jijini Dodoma na ndio maana zimetolewa fedha zaidi ya Tsh 45bn kupelekea upatikanaji wa maji.
"Ninaelekeza wataalamu wa wizara kuhakikisha unafanyika utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji Dodoma Jiji kwa kuchimba visima virefu maeneo mbalimbali.
"Ninaelekeza mitambo ya uchimbaji visima iongezwe hapa Dodoma na ile Timu ya wataalamu waliokuwa kwenye usimamizi wa mradi wa Same Mwanga sasa kuhamia Dodoma mpaka tuhakikishe tunaongeza vyanzo vya kutosha vya maji,"alisema Aweso.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,Mheshimiwa Anthony Mavunde ameshukuru hatua ambazo zinachukuliwa na serikali kukabiliana na upungufu wa maji na kusema miradi hii miwili ikikamilika itaongeza uzalishaji maji kufikia lita 121milioni kwa siku na hivyo kubakisha lita 28milioni kufikia mahitaji ya maji kwa siku.
Akitoa taarifa ya awali,Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Eng. Aron Joseph kukamilika kwa mradi huu kutaleta manufaa kwa wananchi zaidi ya 184,642 katika maeneo ya Nkuhungu, Mkonze, Miganga, Chidachi, Michese,Iyumbu, Mahungu, Ndachi, Njedengwa, Ng’ong’ona, Mlimwa C na Ntyuka kwa awamu ya kwanza.