Afrika tuna nafasi kubwa kustawi kiuchumi-Balozi Mpungwe

NA GODFREY NNKO 

BARA la Afrika bado lina bafasi kubwa ya kupiga hatua kiuchumi katika sekta mbalimbali kutokana na wingi wa rasilimali za asili zilizopo ikiwemo nguvu na rasilimali watu wa kutosha.Hayo yamesemwa leo Mei 24,2025 na Balozi Ami Ramadhan Mpungwe kutoka Wakfu wa Thabo Mbeki (Thabo Mbeki Foundation) katika Mhadhara wa 15 wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki (The Thabo Mbeki 15th Africa Day Lecture) unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Katika mhadhara huo, Balozi Mpungwe amesema kuwa, ili rasilimali hizo ziweze kuleta matokeo bora zinahitaji usimamizi mzuri huku akisisitiza kuwa, msingi wa kuyafikia maendeleo endelevu ni kuhakikisha suala la amani, umoja na mshikamano linapewa kipaumbele kikuu.

Mhadhara wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki ni tukio la kila mwaka linaloandaliwa na Thabo Mbeki Foundation (TMF) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (Unisa) kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Afrika.

Ni siku ambayo huadhimisha kuanzishwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) Mei 25, 1963, huko Addis Ababa, Ethiopia.

Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 62 tangu kuanzishwa kwa OAU, ambayo ndiyo chimbuko la Umoja wa Afrika (AU) uliozinduliwa rasmi huko Durban, Afrika Kusini mwaka 2002.

Uamuzi wa kuandaa Mhadhara wa 15 wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki nchini Tanzania mwaka huu unatokana na mchango mkubwa wa Tanzania katika historia ya bara la Afrika ukiwa umejengwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa Tanzania, mhadhara huu umeandaliwa na Wakfu wa Thabo Mbeki,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (Unisa) ukiangazia mshikamano wa Bara la Afrika na ari ya kujijenga upya.

Profesa Puleng LenkaBula, Mkuu wa Chuo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (Unisa) amesema kuwa,elimu ni msingi muhimu katika kuwezesha ukuaji,maendeleo na ustawi wa Bara la Afrika.

Mbali na Rais Mstaafu Thabo Mbeki ambaye ameshiriki mhadhara huu, pia umewakutanisha viongozi na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news