PWANI-Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb), amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekamilisha taratibu zote na kutoa ruzuku kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Yas kwa ajili ya ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Kimaramisale, Kata ya Dutumi, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Naibu Waziri Mahundi ameyasema hayo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Wilaya ya Kibaha, ambapo alitembelea Kata ya Dutumi ili kujionea changamoto zilizopo na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
“Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tayari imeingia makubaliano na Kampuni ya Yas kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana katika eneo hili. Kwa mujibu wa mkataba huo, mnara unatarajiwa kujengwa na kukamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu,” alisema Naibu Waziri Mahundi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson John, amesema zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa wilaya hiyo wananufaika na huduma za mawasiliano kupitia minara takribani 35 iliyopo. Aliongeza kuwa, kuongezwa kwa mnara huo mpya kutazidi kuimarisha huduma hizo na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya hiyo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Mhe. Raphael Mwakamo, aliwahakikishia wananchi kuwa taratibu zote za ujenzi wa mnara huo zimekamilika. Aidha, aliipongeza Serikali kwa juhudi za kuimarisha huduma za mawasiliano, hususan maeneo ya pembezoni.
Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Yas, Mhandisi Smprius Komba amesema kuwa kampuni hiyo tayari, imepokea zaidi ya asilimia 50 ya ruzuku kutoka UCSAF, na tayati taratibu zote za upatikanaji wa vibali zimekamilika. Amebainisha kuwa ujenzi wa mnara huo utaanza ndani ya wiki moja na utakamilika ndani ya miezi mitatu kama ilivyopangwa.
