Rais Chapo atembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kilichopo Dar

DAR-Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Chapo, amefanya ziara ya kihistoria kwenye Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika, kutazama kumbukumbu za ukombozi zilizotumiwa na wapigania uhuru wa nchi za Afrika zilizohifadhiwa kituoni hapo.
Rais Chapo akiongozwa na Waziri wa Habari, utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ametembelea makumbusho ya kituo hicho kilichobeba historia na uhusiano mkubwa wa kisiasa ulioanziwa na viongozi wa harakati za ukombozi, Mwalimu Julius Nyerere na Samora Machel kilichopo jijini Dar es Salaam, leo Mei 8, 2025.

Katika makumbusho hiyo Rais Mhe. Chapo ametazama vielelezo vya picha, nyaraka na vifaa vya kihistoria vilivyotumika katika harakati za kupigania uhuru pamoja na kuzindua picha ya kihistoria iliyohifadhiwa kituoni hapo.
Aidha, Rais Chapo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka juhudi za kuhifadhi na kurithisha historia ya ukombozi.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amebainisha kuwa majengo ya Kituo hicho yalikuwa ni kitovu cha harakati za ukombozi na Makao makuu ya ofisi za Kamati ya Ukombozi wa Nchi huru za Afrika (OAU Liberation Committee), iliyosaidia kuratibu uhuru wa nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Msumbiji kwa kukisaidia chama cha FRELIMO kilichoongozwa na Samora Machel misaada mbalimbali ikiwemo silaha, fedha na diplomasia kwa kipindi cha mapambano hadi walipopata uhuru wa nchi mnamo tarehe 25, Juni 1975.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news