Samia Innovation Fund mbioni, kuwezesha wabunifu kupata mikopo nafuu

DODOMA-Serikali inatarajia kuanza utekelezaji wa mfuko wa Ubunifu wa Samia “SAMIA Innovation Fund” wenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3 utakaotoa mikopo nafuu kwa wabunifu kwa lengo la kuendeleza na kubiasharisha ubunifu pamoja na kutoa fursa za ajira kwa watanzania kupitia kazi za ubunifu.Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda (Mb) amebainisha hayo Mei 12,2025 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo.

Amesema kuwa lengo la mfuko huo itakuwa ni kuimarisha ubora wa kazi za watafiti na kukuza ushindani wa kitaaluma.
Pia, amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa tuzo yenye thamani ya Shilingi milioni 50 kwa utafiti utakaochapishwa katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa ili kuwahamasisha watafiti na wabunifu kuchapisha na kusambaza matokeo ya kazi zao na kuweza kutumika na wananchi.

Vilevile, Waziri Mkenda amesema kuwa ili kuendana na mabadiliko ya sayansi, teknolojia na ubunifu kikanda na kimataifa, Serikali itaendelea na mapitio ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (1996) ili kuwa na sera inayoakisi hali halisi na mahitaji ya sasa katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

Waziri Mkenda amesema, serikali itafanya tathmini ya Sera ya Taifa ya Utafiti na Maendeleo 2010, Sera ya Taifa ya Bioteknolojia 2010 na Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia 2013 ili kubaini hali halisi ya utekelezaji wa sera hizo.
Wabunifu na kazi za ubunifu ni chachu katika kuzalisha teknolojia mpya, kutatua changamoto za kijamii na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news