Tanzania na Msumbiji kuimarisha ushirikiano katika Diplomaisa ya Uchumi

DAR-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), kwa kushirikiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Maria Manuela Dos Santos Lucas, wameongoza kikao maalumu cha mawaziri wanaoshughulikia sekta za kiuchumi na uchukuzi kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.Kikao hicho kilichohudhuriwa na Mawaziri wa Viwanda na Biashara, Uwekezaji, uchukuzi na masuala ya Uchumi kutoka Tanzania na Msumbiji pamoja na Mabalozi wake wa pande zote; kimejadili maeneo zaidi ya ushirikiano baina ya nchi hizo ili kuimarisha uhusiano wa uwili na kukuza diplomasia ya uchumi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kombo alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Msumbiji kuanzisha miradi ya ubia katika sekta za biashara na uwekezaji, miundombinu ya uchukuzi, nishati, madini, kilimo, viwanda, maendeleo bandari na maeneo maalum ya kiuchumi; hatua itakayoimarisha ushrikiano wa uwili na diplomaisa ya Uchumi kati ya mataifa hayo.

Mhe. Kombo pia alipendekeza kuundwa Kamati ya Pamoja ya Kiufundi itakayokuwa jukwaa la majadiliano ya sera za kiuchumi na ufuatiliaji wa miradi ya pamoja iliyokubaliwa kati ya Tanzania na Msumbiji kupitia mikataba au hati za makubaliano ya ushirikiano katika maeneo husika.

“Ushirikiano wetu unapaswa kulenga kuondoa vikwazo vya biashara kama gharama kubwa za miamala, ucheleweshaji wa mizigo mipakani, utofauti wa kanuni, na ukosefu wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo. Tunapaswa kuratibu sera, kurahisisha taratibu za forodha na usalama wa mimea, na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika nyaraka za biashara,”alisisitiza Mhe. Kombo.

Mhe. Kombo pia alitahadharisha kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo uonekane katika ongezeko la biashara, kuongezeka kwa uwekezaji wa pamoja, na mafanikio yanayopimika kwa maendeleo ya watu wa pande zote.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Maria Manuela Dos Santos Lucas, alisisitiza umuhimu wa kuandaa mpangokazi wa pamoja na wa kimkakati utakaowezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuchochea ushirikiano endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news