DAR-Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Bw. Lazaro Twange amesema wananchi wa maeneo ya Mbagala na viunga vyake sasa wanatarajia kupata umeme wa uhakika baada ya Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mbagala kuongezewa uwezo kutoka Megawati 45 za awali na kufikia Megawati 165.

“Kituo hiki kimeongezewa uwezo mara mbili ya awali na mpaka sasa utekelezaji wa Mradi huu umefikia asilimia 70. Wananchi wa Mbagala na viunga vyake sasa wategemee umeme wa uhakika,’’alisisitiza Bw. Twange.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sixtus Mapunda, akizungumza wakati wa ziara hiyo amepongeza jitihada zinazofanywa na TANESCO ambapo amefafanua kuwa kukamilika kwa Mradi huo kutasaidia kumaliza kero ya umeme katika maeneo mengi ya Mbagala, Temeke na Mkuranga.

Uboreshaji wa Mradi huu wa Kituo cha Kupokea na Kupoza na Kusambaza umeme cha Mbagala umegharimu Dola za Kimarekani milioni 6.4 ambapo sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake na kukamilika kwake kunatarajia kusambaza umeme wa Megawati 165.