Usomaji wa Shahada ya Uzamili ya Kiswahili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania-2

Sehemu ya Pili

Wapendwa wanafunzi na waombaji wapya, awali ya yote tunapenda kutumia fursa hii kuwapongeza na kuwakaribisha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Ufundishaji na Ujifunzaji katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni Nyumbufu kiasi kwamba inakufanya kuwa huru katika kutafuta maarifa, ujuzi na uzoefu kupitia mifumo mbalimbali ya kisasa ya TEHAMA.

Wapendwa wanafunzi na waombaji wapya

Programu ya Uzamili ya Kiswahili hufunzwa kwa muda wa miezi 18 na kuendelea mpaka miaka mitano kutegemea na nafasi ya mwanafunzi pia uwezo wake wa kulipia masomo yake.

Kimsingi, Programu ina jumla ya Vigezi (Units) 18 ikiwa ni sawa na Vigezi 12 vya masomo ya darasani na Vigezi 6 ya Uandishi wa Tasinifu.

Vigezi 12 vya Darasani hujumuisha masomo 6 yenye Vigezi 2 kila kimoja. Ada ya Kigezi kimoja ni 180,000/= fedha za Tanzania.

Ada ya Programu nzima ni 180,000×18+Michango inakuwa ni 3,560,000/= kwa miaka yote mwanafunzi atakayosoma ndani ya kipindi cha uhai wa uanafunzi cha miaka 5.

Hivyo basi, mwanafunzi hushauriwa kuanza na Vigezi 4 mpaka 6 kutegemea na uwezo wake. Ambapo atasoma kwa miezi 4 mpaka 5 kisha anafanya Mitihani na baadae anaendelea na Vigezi vingine vilivyobaki.

Hata hivyo, mwanafunzi ambaye anapenda kuanza na Vigezi 2 anaruhusiwa ingawa itamchukuwa muda mrefu kumaliza Tamrini yake.

Kimsingi, maelezo haya yanaonesha kuwa katika kipindi cha Miezi 8 mpaka Miezi 12 mwanafunzi atakuwa amemaliza masomo ya darasani na kuingia katika Utafiti na Uandishi wa Tasinifu.

Wapendwa wanafunzi na waombaji wapya

Naomba sasa niwatajie kozi ambazo zinafundishwa katika Programu ya Shahada ya Uzamili katika Kiswahili. Programu hii ina makundi mawili ya Ubobezi ambayo ni Fasihi na Isimu.

FASIHI

Katika kundi hili kunafundishwa kozi za:

OSW 601: Ushairi wa Kiswahili

OSW 602: Tamthiliya ya Kiswahili

OSW 603: Riwaya ya Kiswahili

0SW 604: Nadharia za Fasihi na Uhakiki

OSW 606: Fasihi Simulizi

OSW 616: Mbinu za Utafiti

Hizi ndizo kozi za lazima kwa wanafunzi wote wanaosoma Shahada ya Uzamili ya Kiswahili mkondo wa Fasihi. Kila kozi ina Vigezi 2.

Ukitazama Prospectus utaona kozi nyingine za Hitiari na unaruhusiwa kusoma kama unapenda na kufanya malipo.

ISIMU

Katika mkondo huu kozi zinazofunzwa ni:

OSW 608: Fonetiki na Fonolojia ya Kiswahili

OSW 609: Mofolojia ya Kiswahili

OSW 610: Sintankisia ya Kiswahili

OSW 611: Semantiki ya Kiswahili

OSW 613: Isimu Jamii

OSW 616: Mbinu za Utafiti

Hizi ndizo kozi za Darasani ambazo husomwa na wanafunzi wa mkondo wa Isimu na kila kozi ina Vigezi 2.

Ukitazama kwenye Prospectus utaona kozi nyingine za Hitiari ambazo unaruhusiwa kusoma ikiwa unapenda na kufanya malipo stahiki.

UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI

Katika Programu hii tunafundisha na kujifunza kwa kutumia mfumo wa Moodle, Mihadhara kwa njia ya ZOOM na Ana kwa Ana.

Kupitia mifumo hii ambayo tutawapatia mafunzo ya kuitumia mtaweza kujinoa na kuwa wabobezi katika masomo yenu.

Mifumo hii itawapatia fursa ya kujifunza zaidi kupitia majadiliano ya vikundi na pia usomaji wa binafsi.

KUHUSU UPIMAJI

Kimsingi, upimaji unafanywa kwa Mazoezi, majaribio, kazi za vikundi na Uandishi wa Insha ya Muhula kwa kila somo.

Haya hufanyika katika kipindi chote cha Ufundishaji na Ujifunzaji. Kazi hizi hutengeneza Alama 50 na Kisha Mtihani wa mwisho ambao nao huwa na Alama 50 na kufanya jumla ya Alama 100 kwa kila kozi. Ufaulu ni Alama 50.

Hivyo, ni wajibu wa Mwanafunzi kuzingatia maelekezo ya Mwalimu wa kozi na kufanya kazi zote anazopewa ili aweze kutimiza matakwa ya Upimaji wa Programu hii ya Shahada ya Uzamili ya Kiswahili.

Maelezo ya kina juu ya usomaji yapo katika andiko linaloitwa Usomaji wa Shahada ya Uzamili ya Kiswahili Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

UANDISHI WA TASINIFU

Mwanafunzi anapomaliza kozi za Darasani anasajili Vigezi vya Tasinifu ambayo ni:

OSW 617: Uandishi wa Tasinifu

Baada ya kusajili atapangiwa msimamizi wa kumuoongoza katika Utafiti wake. Mwanafunzi atafanya Utafiti wake kwa kuzingatia miongozo yote ya Chuo ambayo imeanishwa kwenye Prospectus ya chuo.

ULIPAJI WA ADA

Tayari nimeshaeleza hapo awali kwamba Ada ya Chuo ni kiasi gani. Sasa ili kufanya malipo, mwanafunzi anatakiwa kusajili kozi kwa muongozo niliyoutoa wa kwamba ni Vigezi vingapi vya kuanzia na pia nikasema hata Vigezi 2 mwanafunzi anaweza kusajili, kulipia na kuanza masomo yake.

Baada ya kusajili utapata Invoice na Kisha Control Number ya kufanyia Malipo. Ada ya Chuo hailipwi mkononi wala Cash kwa mtu yeyote, awe Mratibu kama Mimi, Mkuu wa Idara, mwalimu wa Somo au mfanyakazi yeyote wa Chuo.

Fedha za Chuo zinalipwa kwa Control Number. Zingatia maelekezo haya ili fedha zako zisipotee na baadae ukajikuta unadaiwa na Chuo.

Kwa wanafunzi wapya, maombi yanapokelewa kupitia www.out.ac.tz au fika kituo cha karibu cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania utahudumiwa.

HITIMISHO

Kwa hakika, katika andiko hili fupi tumeeleza mengi, itoshe tu kusema kwamba, tunawapenda sana Wanafunzi wetu na tunawaomba mjitume katika masomo ili muweze kukamilisha na kuhitimu kwa muda uliopangwa.

Mawasiliano na walimu ni jambo muhimu na pale unapokumbana na changamoto yoyote basi usisite kuwasiliana na Mratibu, Mkuu wa Idara na Mwalimu wa Somo husika ili changamoto hiyo itatuliwe.

Ujifunzaji kwa njia ya Huria na Masafa unahitaji nidhamu ya hali ya Juu ili kufikia malengo. Ni matumaini yetu kwamba mtazingatia maelekezo haya.

TUMA maombi yako kabla ya tarehe 30/05/2025.

Karibuni sana

WENU,

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mratibu wa Programu
Umahiri Kiswahili
22/04/2025

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news