RUKWA-Watu sita wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa baada ya daladala yenye namba za usajili T 294 DSS inayofanya safari zake kati ya vijiji vya Sikaungu-Malonje wilayani Sumbawanga kuigonga pikipiki ya magurudumu matatu maarufu kama bajaji.
Ni yenye namba za usajili MC 416 BZQ iliyokuwa imeegeshwa kando ya barabara katika eneo la Ulinji nje kidogo ya mji wa Sumbawanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Shadrack Masija amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo taarifa za awali zinaonesha kuwa, ilisababishwa na hitilafu katika mfumo wa breki au dereva kutumia mwendo huru (neutral) katika eneo hatarishi lenye mwinuko mkali.

Sambamba na majeruhi 21 wakiwemo wanawake 8 na wanaume 13 huku watatu kati yao wakiwa katika hali ya mahututi katika wodi ya uangalizi maalum (ICU).
Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere,Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ametoa salamu za pole kwa familia zote za wafiwa, ndugu,jamaa na marafiki wa wahanga wote na kuwatakia uponyaji wa haraka majeruhi wote.
