Ajali yaua 37 na kujeruhi 29 wilayani Same

KILIMANJARO-Watu 37 wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali mbaya jioni ya Juni 28,2025 wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo imetokea katika eneo la Sabasaba, kata ya Same, na imehusisha basi la kampuni ya Channel One lenye namba za usajili T 179 CWL lililokuwa likitoka Moshi kuelekea Tanga kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Coaster lenye namba za usajili T 199 EFX lililokuwa likitoka wilayani Same, na magari yote mawili yamewaka moto.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ambaye ametembelea eneo la tukio na kuwatembelea majeruhi hospitalini, amesema ajali kama hiyo haijawahi kutokea mkoani humo na kuitaja kama msiba mkubwa kwa taifa.

“Mpaka sasa Watanzania 37 wamefariki, tunao majeruhi 29 ambapo 24 wapo hapa katika Hospitali ya Mji Same na wengine watano wamekimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi na KCMC kwa kweli ni msiba mkubwa,” amesema Mhe. Babu.

Ameongeza kuwa serikali imeanza utaratibu wa upimaji wa vinasaba (DNA) kwa miili ya marehemu ili iwe rahisi kutambua ndugu na jamaa zao kutokana na miili hiyo kuungua vibaya na kutotambulika kirahisi.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewaomba wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za ndugu zao ambao hawajawaona kuanzia leo ili kujiridhisha kwa kuwa bado kuna miili haijatambuliwa.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro SACP Simon Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la basi la kampuni ya Channel One lililokuwa likitoka Moshi kuelekea Tanga na kusababisha basi hilo kupoteza mwelekeo na kugongana uso kwa uso na Coaster, kabla ya magari yote kuwaka moto."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news