NA LWAGA MWAMBANDE
JUMATANO ya wiki hii,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, nchi za Afrika zinapaswa kuzingatia kujipatia uhuru kamili wa kiuchumi.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesisitiza kwamba, uhuru wa kisiasa uliopatikana kwa kuvuja jasho, ni hatua ya kwanza tu katika safari ndefu zaidi kuelekea ustawi na heshima barani Afrika.
Ameyasema hao mjini Maputo,Msumbiji alipokuwa mgeni wa heshima katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Msumbiji, akitilia mkazo kwamba bara hilo lazima sasa lielekeze nguvu zake za pamoja katika kukomboa uchumi wake.
Vilevile kuimarisha biashara ya kikanda na kukuza uwekezaji wa ndani ya Afrika.
Rais Dkt.Samia amesema, maono ya waasisi wa bara hilo sio tu kufuta utawala wa kikoloni bali pia kuunda jamii zinazojitegemea, zenye ustawi na zilizojikita katika utu, usawa na fursa, hivyo kizazi cha leo kinapaswa kurithi na kukamilisha kazi hiyo.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, mfanikio ya kiuchumi yanahusisha uwezo wa kudhibiti mapato, matumizi na uwekezaji ili kufikia uhuru wa kifedha na maisha bora kwa wote, huku akibainisha usimamizi thabiti wa rasilimali zilizopo Afrika ni majawabu tosha ya kufikia Uhuru wa Kiuchumi. Endelea;
1. Ni miaka ya sitini, ilisemwa lugha hii,
Kuondoka mkoloni, kwa zile zetu bidii,
Hilo jambo la thamani, zama hadi leo hii,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
2. Uhuru wa kiuchumi, hiyo ni vita nyingine,
Na ni vita haikomi, yajigeuza vingine,
Bara letu hatuvumi, wanaotamba wengine,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
3. Katika vitu vinne, vya kututoa tulipo,
Vema tujadiliane, ni wapi sisi hatupo
Na halafu tupambane, ili na hapo tuwepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
4. La kwanza wawepo watu, hilo tiki sisi tupo,
Watu walojaa utu, na wasio utu wapo,
Bilioni hii yetu, ni idadi kubwa ipo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
5. Jambo la pili ni ardhi, hiyo kubwa sana ipo,
Juu njema sana ardhi, kilimo mifugo ipo,
Hata chini tuna hadhi, utajiri mwingi upo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
6. Hivi ni madini gani, barani kwetu hayapo,
Mengi sana ya thamani, hata uhitaji upo,
Lakini hivi kwanini, kwenye uchumi hatupo?
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
7. Tatu ni siasa safi, hivi kweli hiyo ipo,
Au ishakuwa ghafi, na uzalendo haupo,
Tunapigana makofi, na ubishi upoupo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
8. Kama ubepari upo, pia ujamaa upo,
Wanamapinduzi upo, na uhafidhina upo,
Na nyingine ipoipo, kujulikana hakupo,
Bado tunapambania Uhuru wa kiuchumi.
9. Nne uongozi bora, Afrika yetu haupo,
Nchi nyingi unakera, demokrasia haipo,
Kwa uchumi ni hasara, mafanikio hayapo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
10. Vita wenyewe wenyewe, tunavyopigana vipo,
Zitaje nchi mwenyewe, karibia kote vipo,
Twajimaliza wenyewe, na utulivu haupo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
11. Sudani na Somalia, mapigano bado yapo,
Sudani Kusini pia, kusigana kupokupo,
Nani anaangalia, heri uchumi iwepo?
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
12. Hapo sijasema Kongo, na huko uasi upo,
Wenyeji ni lao zogo, wageni mavuno yapo,
Sisi sawa na utingo, umatemate haupo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
13. Nenda kule magharibi, utajiri mwingi upo,
Lakini hatuukabi, maendeleo yawepo,
Ni wale wa Magharibi, ni faida kubwa ipo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
14. Hapa sasa twatokaje, ili Uhuru uwepo,
Hasahasa tufanyeje, kunyanyaswa kusiwepo,
Au nani tumngoje, kwamba mkombozi yupo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
15. Vema tujitafakari, mabadiliko yawepo,
Kwa uongozi mzuri, kujali watu kuwepo,
Tena sana kufikiri, maendeleo yawepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
16. Wageni kunyenyekea, huko wala kusiwepo,
Wenyeji kupotezea, rushwa hiyo isiwepo,
Tuweze kujitetea, matunda kwetu yawepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
17. Wanaotugombanisha, na amani isiwepo,
Hapo vema kufurusha, nafasi kwao haipo,
Tuishi yetu maisha, amani kwetu iwepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
18. Umimi ukiondoka, mpenyo utakuwepo,
Ila bila kuondoka, utumwa utakuwepo,
Ya wengine tutashika, hata kwa kula viapo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
19. Nyerere angefufuka, na Nkurumah ngekuwepo,
Lumumba twamkumbuka, Na Sankara ngekuwepo,
Tungekuwa tumefika, pengine kwenye uwepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
20. Na endapo kila mtu, aweza kula kiapo,
Kwamba atatumika tu, maendeleo yawepo,
Bila ya tuvituvitu, tutafika penginepo,
Bado tunapambania Uhuru wa kiuchumi.
21. Hivi kweli tutafika, ni bora swali liwepo,
Kitu tuweze kushika, na uoga usiwepo,
Tutakapo weze fika, utajiri mwingi upo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
22. Vinginevyo tutabaki, tunazunguka tulipo,
Ya watu tunalaiki, yetu twawa tupotupo,
Tukienda hatufiki, hadi kiama kiwepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
23. Endapo kuna mlozi, wasema ulozi upo,
Twapaswa kufanya kazi, kutangua usiwepo,
Na sisi tupande ngazi, tuwafikie walipo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
24. Kasema Mama Samia, Uhuru uzidi wepo,
Uchumi kupambania, ni lengo kuu liwepo,
Hili twamkubalia, nia lazima iwepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
25. Nguvu kuzielekeza, kwenye uchumi ziwepo,
Kujikomboa twaweza, umoja wetu uwepo,
Mtangamano kukuza, kwa kanda zetu kuwepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
26. Biashara kati yetu, bara Afrika uwepo,
Hizi jitihada zetu, uwekezaji uwepo,
Kina Dangote wenzetu, na wengiwengi wawepo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
27. Kweli Rais Samia, amani budi iwepo,
Muda tukiutumia, uzalishaji uwepo,
La tutazidi kulia, tukibakia tulipo,
Bado tunapambania, Uhuru wa kiuchumi.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
