Bunge laidhinisha shilingi trilioni 20.19 za Wizara ya Fedha,kutekeleza vipaumbele vitano

NA GODFREY NNKO

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameidhinisha shilingi trilioni 20.19 kwa ajili ya bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Ni saa chache baada ya leo Juni 4,2025 bungeni jijini Dodoma Waziri wa Fedha, Mhe.Dkt.Mwigulu Nchemba kuwasilisha Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2024/25 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka 2025/26.

Dkt.Nchemba amelieleza Bunge kuwa, kupitia bajeti ya mwaka ujao wizara yake inatarajia kutekeleza vipaumbele vitano ikiwemo kutafuta na kukusanya mapato ya jumla ya shilingi trilioni 50.98 kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya serikali.

Amesema,kati ya kiasi hicho, Mamlaka yaMapato Tanzania inatarajiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 34.10, misaada shilingi trilioni 1.07, mikopo nafuu na ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani na nje shilingi trilioni 14.95 na maduhuli shilingi bilioni 53.54.

Waziri Dkt.Nchemba amesema,pia Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inakadiriwa kukusanya shilingi milioni 843, ikiwa ni ukodishaji wa kumbi za mikutano na kodi ya pango kutokana na upangishaji wa majengo ya ofisi yaliyopo katika mikoa mbalimbali nchini.

Pili, Dkt.Nchema amesema, wanatarajia kuhudumia kwa wakati deni la serikali linalotarajiwa kuiva la jumla ya shilingi trilioni 14.22.

Tatu,amesema wanatarajia kujenga mfumo wa pamoja wa kutoa ankara za malipo ya serikali ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Kipaumbele cha nne ni kuboresha, kuunganisha na kuimarisha usalama wa mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha na mali za umma na tano ni kuandaa Sera ya Usimamizi wa Mali za Umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news